UFARANSA-UGAIDI

Disneyland Paris: mtu mmoja akamatwa na silaha, mwenzake asakwa

Mbele ya lango la  hoteli ya Hifadhi ya pumbao ya Disneyland Paris, Agosti 13, 2016.
Mbele ya lango la hoteli ya Hifadhi ya pumbao ya Disneyland Paris, Agosti 13, 2016. AFP/AFP

Mtu mmoja na silaha mbili pamoja na Koran Takatifu amekamatwa Alhamisi hii katika hoteli ya Hifadhi ya pumbao ya Disneyland Paris (Seine-et-Marne), mashariki mwa mji mkuu wa Ufaransa, na mwenzake anasakwa, vyanzo vya polisi vimebaini.

Matangazo ya kibiashara

Mtu huyo "amegunduliwa alipowasili katika hoteli ya Disneyland ambako alikua amelipia chumba", chanzo cha polisi kimeliambia shirika la habari la Ufaransa AFP.

"Kengele ya tahadhari ilisikika alipokua akipita sehemu mojawepo ya hoteli ya Disneyland", chanzo kingine kimebaini.

"Maafisa wa usalama katika hoteli ya Disneyland walimkuta mtu huyo akiwa na silaha mbili, Koran Takatifu pamoja na risase nyingi", chanzo cha kwanza cha polisi kimeendelea. Ikiitwa kwenye eneo la tukio, polisi ilimkamata mtu huyo mapema mchana na kumuwekwa chini ya ulinzi.

Eneo la usalama limetengwa pembezoni mwa gari lake, chanzo hicho kimeongeza.

Mtu mwengine aliyekua akiambatana na mtu huyo anatafutwa na wachunguzi, kwa mujibu wa chanzo cha polisi.

Mtu huyo ambaye ni mkazi wa mji Paris kulingana na vyeti alivyokuwa navyo, amewekwa chini ya ulinzi katika gereza la polisi ya mji wa Versailles, ambayo imeanzisha uchunguzi.

Maelezo kuhusu mtu huyo hayajatolewa hadi sasa.

Ufaransa inaishi chini ya tishio la mashambulizi ya kigaidi baada ya mashambulizi ya mwezi Januari na Novemba 2015.