SYRIA-GENEVA-UN

Mazungumzo ya amani kuhusu Syria yang'oa nanga mjini Geneva huku pinzani ukisuasua kushiriki

Ujumbe wa Serikali ya Syria ukiwa mjini Geneva
Ujumbe wa Serikali ya Syria ukiwa mjini Geneva REUTERS/Goran

Mjumbe maalumu wa umoja wa Mataifa kuhusu Syria, anakabiliwa na changamoto kubwa ya kuhakikisha mazungumzo ya amani kumaliza mzozo wa nchi hiyo yaanza kwa wakati mjini Geneva hii leo, wakati huu upinzani ukisitasita kushiriki mazungumzo na utawala wa Damascus.

Matangazo ya kibiashara

Mazungumzo ya dharura kuhusu kupata suluhu ya mzozo wa Syria uliodumu kwa zaidi ya miaka minne, yalifufuliwa tena mwishoni mwa juma, huku kukiripotiwa milipuko iliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 70 jirani na msikiti wa waumini wa kishia nje kidogo ya mji mkuu Damascus.

Makundi ya kiislamu yamekiri kuhusika na milipuko ya siku ya Jumapili, ambapo makundi haya yamekuwa yakifanya kazi kusini mwa Syria na Iraq ambapo yamezidisha mashambulizi dhidi ya raia.

Mkuu wa sera za mambo ya kigeni wa umoja wa Ulaya, Federica Mogherini, amesema kuwa mashambulizi yanayotekelezwa wakati huu nchini Syria, yanalenga kubadili uelekeo wa mazungumzo ya Geneva.

Vifo vya mwishoni mwa juma vinafanya idadi ya watu waliouawa mpaka sasa nchini Syria, kufikia waty laki 2 na elfu 60 toka mwaka 2011.

Miongoni mwa watu wanaoshiriki mazungumzo ya Geneva, ni pamoja na muungano mkuu wa upinzani nchini Syria na wawakilishi wa utawala wa rais Bashar al-Asad.

Chini ya mkataba uliotiwa saini mjini Vienna mwezi November mwaka jana, na kukubaliwa na pande zinazohusika kwenye mzozo huo, ni kuwa na mazungumzo ya kina ambayo hata hivyo huenda yasiwe ya ana kwa ana na yatakayodumu kwa zaidi ya miezi 6.

Makubaliano hayo ya awali yanataka kufanyika kwa uchaguzi mkuu katika kipindi cha miezi 18, lakini swali kuu linabaki ni kwa vipi rais Asad atashiriki katika mchakato huo, hatua inayoungwa mkono na Urusi pamoja na China.