SYRIA-MAREKANI-UFARANSA-UN

Marekani na Ufaransa zautuhumu utawala wa Syria na Urusi kwa kukwamisha juhudi za mazungumzo ya amani ya Syria

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry (Kushoto) akiwa na mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov (Kulia)
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry (Kushoto) akiwa na mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov (Kulia) REUTERS/Goran

Marekani na Ufaransa zinamtuhumu rais wa Syri, Bashar al-Assad na utawala wake kuwa chanzo cha kudumaza mazungumzo ya amani kumaliza mzozo wa nchi yake, mazungumzo ambayo yameahirishwa saa chache kabla ya nchi wafadhili wa Syria kukutana alhamisi hii kuongeza msaada zaidi kwenye nchi hiyo yenye vita. 

Matangazo ya kibiashara

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa, Laurent Fabius, anaituhumu Serikali ya Damascus na Urusi, kwa makusudi kudumaza juhudi za mazungumzo ya amani, baada ya kuanzisha mashambulizi mapya ya anga kwenye mji wa Aleppo, akiongeza kuwa dunia inapaswa kuwa na mazungumzo ya kina zaidi wakat nchi wafadhili zitakapokutana.

Umoja wa mataifa umelazimika kuahirisha mazungumzo haya yaliyoonekana kama yangetoka na maazimio mazuri hapo jana, wakati huu utawala wa Sryria ukidai kuwa umefanikiwa kukata mawasiliano na njia kuu zinazotumiwa na waasi katika mji wa pili kwa ukubwa jirani na nchi ya Uturuki kwa msaada wa mashambulizi ya ndege za Urusi.

Haya ni mashambulizi makubwa zaidi kuwahi kutekelezwa na majeshi ya Sryria na Urusi ambapo waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Sergei Lavrov amesema hakuona sababu ya nchi yake kuacha kutekeleza mashambulizi hadi pale magaidi watakaposhindwa.

Mpatanishi wa umoja wa Mataifa kwenye mzozo wa Syria, Staffan de Mistura
Mpatanishi wa umoja wa Mataifa kwenye mzozo wa Syria, Staffan de Mistura Reuters/路透社

Mazungumzo ya safari hii yalitajwa kama moja ya hatua muhimu na yenye tija kuelekea kumaliza machafuko ya nchini Syria, machafuko yaliyodumu kwa karibu miaka mitano hivi sasa, huku watu zaidi ya laki 2 na elfu 60 wakiuawa na wengine maelfu wakikimbia nchi yao.

Hata hivyo mazungumzo haya yanaonekana kukwama hata kabla ya kushika kasi, huku upinzani unaoshiriki kwenye mazungumzo hayo ukidai kuwa hautarejea tena mjini Geneva hadi pale utawala wa Damascus utakapokubali kusitisha mashambulizi kwenye miji yenye vita.

Mpatanishi wa mzozo wa Syria, Staffan de Mistura amesema kuwa mazungumzo mengine yatafanyika February 25, akisisitiza kuwa kuahirishwa kwa mazungumzo haya sio mwisho wa mazungumzo zaidi na kutoa wito kwa wadau wa mzozo huo kufanya jitihada zaidi ili kufikia malengo.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, John Kerry amesema kuwa utawala wa Syria unalenga kuchukua maeneo zaidi huku mazungumzo yakiendelea hatua inayodhihirisha namna ambavyo utawala huo hautaki kuona amani ya kudumu inapatikana kwa njia ya mazungumzo.

Kerry amesema kuwa kuendelea kwa mashambulizi yanayofanywa na utawala wa Syria wakisaidia na Urusi dhidi ya ngome zinazoshikiliwa na upinzani, ni wazi inatoa ishara ya nchi hizo kutaka kutumika kwa nguvu za kijeshi zaidi kuliko diplomasia.