UBELGIJI-MASHAMBULIZI-UGAIDI

IS yadai kuhusika na mashambulizi ya Brussels

Polisi ikitoa ulinzi mbele ya kituo cha treni baada ya mashambulizi yalioukumba mji mkuu wa Ubelgiji, tarehe 22 mars.
Polisi ikitoa ulinzi mbele ya kituo cha treni baada ya mashambulizi yalioukumba mji mkuu wa Ubelgiji, tarehe 22 mars. REUTERS/Christian Hartmann

Kundi la Islamic State kupitia shirika lake la habari la AMAQ, limekiri kuwa limehusika katika mashambulizi yaliotokea katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Zaventem na katika kituo cha treni za mwendo wa kasi mjini Brussels. Taarifa hii imethibitishwa na tovuti maalum ya Marekaniya SITE.

Matangazo ya kibiashara

Wakati huo huo serikali ya Ubelgiji imetangaza Jumanne hii maombolezo ya kitaifa ya siku tatu baada ya mashambulizi katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Zaventem na katika kituo cha treni za mwendo wa kasi mjini. Mashambulizi ambayo yaliwaua watu wasiopungua 34 kwa ujumla, kulingana na idadi ya muda iliyotolewa muda mfupi uliyopoita.

Maombolezo haya ya kitaifa yatachukua muda hadi Alhamisi jioni, amesema Frédéric Cauderlier, msemaji wa Waziri Mkuu wa Ubelgiji Charles Michel. "Ni maombolezo ya kipekee, bendera zote za kitaifa zitapandishwa nusu mlingoti katika majengo yote ya serikali," ameongeza. Bendera ya taifa kwenye dirisha la afisi ya Waziri Mkuu imepandishwa nusu mlingoti saa saba mchana saa za Ubelgiji (sawa na saa 12:00 saa za kimataifa).

Mashambulizi hayo yanatokea baada ya siku tatu ya kukamatwa kwa mtuhumiwa mkuu wa mashambulizi ya Paris mjini Brussels, Salah Abdeslam. Mashambulizi yaliogharimu maisha ya watu 130 na wengine wengi kujeruhiwa.

Baada ya mashambulizi hayo katika mji mkuu wa Ubelgiji, Brussels, nchi kadhaa za Ulaya jirani na Ubelgiji zimeimarisha hatua zao za usalama na udhibiti wa mipaka. Ufaransa, Ujerumani na Uholanzi lakini pia Uingereza zimetangaza masharti mapya mara baada ya mashambulizi yaliogharimu maisha ya watu wasiopungua 34.