UFARANSA-HOLLANDE-SIASA-USALAMA

François Hollande aachana na marekebisho ya katiba

Rais wa Ufaransa François Hollande.
Rais wa Ufaransa François Hollande. REUTERS/Stephane de Sakutin/Pool

Baada ya miezi minne ya mijadala mikali, François Hollande Alhamisi hii, ameamua kuachana na marekebisho ya katiba ambayo alianzisha mwenyewe baada ya mashambulizi ya Novemba, na ambayo yalikwama kufuatia suala la kunyang'anywa uraia kwa Wafaransa wenye asili ya kigeni watakaojihusisha na ugaidi.

Matangazo ya kibiashara

"Nimeamua, baada ya kuzungumza na marais wa Bunge na Seneti, kuhitimisha mjadala wa kikatiba," Rais Hollande ametangaza rasmi Jumatano hii katika Ikulu ya Elysee katika tangazo la dakika tano.

Miezi minne baada ya kupongezwa na karibu wabunge wote mjini Versailles, Rais Hollande "anaona leo kwamba Bunge na Seneti wameshindwa kuafikiana na maelewano yanaonekana kutofikia juu ya ufafanuzi wa kunyang'anywa uraia kwa magaidi. "

"Pia naona kwamba sehemu moja ya upinzani inapinga marekebisho yoyote ya kikatiba, ambayo yanahusu hali ya tahadhari au hata uhuru wa vyombo vya sheria. Ninasikitishwa na tabia hii. Kwa maana tunapaswa kufanya chochote kile katika mazingira tunayojua, na ya hatari, ili kuepuka mgawanyiko na kuzuia hali ya sintofahamu ambayo ingeliweza kutokea kwa wakati wowote", Rais Hollande ameeleza. Hata hivyo hakutaja mjadala ulioibua mgawanyiko katika chama cha mrengo wa kushoto na kusababisha kujiuzulu kwa Christiane Taubira, aliyekuwa Waziri wa Sheria.

Wiki iliyopita, Baraza la Seneti lenye wajumbe wengi kutoka mrengo wa kulia,, lilitupilia mbali hoja ya kunyang'anywa uraia kwa Wafaransa wenye asili ya kigeni pekee, ikibaini kwamba hali hiyo inaweza kuzua mkanganyiko na ubaguzi kwa wananchi wa Ufaransa.