UFARANSA-SHERIA ZA KAZI

Wabunge wapiga kura ya kutokua na imani na serikali

Waziri Mkuu wa Ufaransa Manuel Valls, pamoja na Waziri wake wa Kazi, Myriam El Khomri, Bungeni Mei 10, 2016.
Waziri Mkuu wa Ufaransa Manuel Valls, pamoja na Waziri wake wa Kazi, Myriam El Khomri, Bungeni Mei 10, 2016. REUTERS/Charles Platiau

Wabunge nchini Ufaransa wanapiga kura ya kukosa imani ya serikali ya Waziri Mkuu Manuel Valls, kuhusu mswada mpya wa ajira nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Mswada huo umezua maandamano makubwa katika baadhi ya miji nchini humo huku baadhi ya wanasiasa wa upinzani wakisema mswada huo unalenga kuwagawa wafanyakazi wa umma nchini Ufaransa.

Miongoni mwa mapendekezo katika mswada huo ni pamoja na watu kufanya kazi kwa muda wa saa 35 kwa wiki lakini muda huo unaweza kuongezeka kwa saa 46 kwa wiki.

Waajiri wana haki ya kupunguza mishahara ya wafanyakazi, lakini pia kuweka masharti ya kuwafuta kazi wafanyakazi.

Mswada huo pia unazungumzia waajiri kupewa mamlaka ya kuamua ni lini wafanyikazi wanaweza kwenda likizo ikiwa ni pamoja na kwenda kujifungua au kuoa.

Hata hivyo, wachambuzi wa siasa nchini Ufaransa wanasema huenda Waziri Mkuu akaponea kuondolewa lakini chama cha rais Francois Hollande cha Kisosholisti kikiendelea kupoteza umaarufu wakati ambapo ukisalia mwaka mmoja wa uchaguzi Mkuu ambapo umepangwa kufanyika mwezi Mei mwaka ujao.