EU-URUSI

EU yaongeza kwa miezi sita vikwazo dhidi ya Urusi

Jumanne hii, Juni 21 mabalozi kutoka nchi 28 wanachama wa Umoja wa Ulaya wamepitisha uamuzi wa kuongezwa kwa miezi sita vikwazo vikali vya kiuchumi dhidi ya Urusi. Vikwazo hivi vilipitishwa katika majira ya joto mwaka 2014 dhidi ya madai ya kuhusika kwa Urusi katika mgogoro nchini Ukraine.

Wiki iliyopita, Rais wa Urusi Vladimir Putin alisema alitaka kupiga hatua kuelekea nchi za Ulaya, licha ya kuongezwa kwa muda wa vikwazo.
Wiki iliyopita, Rais wa Urusi Vladimir Putin alisema alitaka kupiga hatua kuelekea nchi za Ulaya, licha ya kuongezwa kwa muda wa vikwazo. REUTERS/Vasily Maximov/Pool
Matangazo ya kibiashara

Uamuzi rasmi utachukuliwa bado ili kuongeza muda mpaka Januari 31, 2017 kwa vikwazo ambavyo muda wake unamalizika mwishoni mwa mwezi Julai. Lakini mabalozi ishirini na nane tayari wamepiga kura, kwa mujibu wa vyanzo vilivyohojiwa na shirika la habari la AFP.

Vikwazo hivyo vinaathiri benki na makampuni ya mafuta na ulinzi vya Urusi, na vimeathiri pakubwa uchumi wa Urusi, ambayo kwa upande mwingine ilichukua ikwazo juu ya uagizaji wa chakula kutoka nchi za Umoja wa Ulaya.

Awali, nchi za Umoja wa Ulaya zilipanga kupitisha vikwazo hivi siku ya Ijumaa, ili kutatua suala hili kabla ya mkutano muhimu wa Wakuu wa Nchi na Serikali ambao umepangwa kufanyika tarehe 28 na 29 Juni mjini Brussels, hasa kuhusu madhara ya kura ya maoni ya Uingereza juu ya kusalia au la katika Umjoa wa Ulaya.

Lakini mataifa mawili wanachama, Ufaransa na Uingereza, zinatakiwa kwanza kujulisha mabunge yao, jambo ambalo linaweza kuchelewesha mchakato.

Akiwa ziarani mjini Paris, Rais wa Ukraine Petro Poroshenko amedai kuwa vikwazo hivyo ni "hatua ambayo imekua imesalia" kwa kuiwekea shinikizo Urusi na kuilazimisha kuheshimu makubaliano ya amani yaliyoafikiwa mjini Minsk.

Paris na Berlin, ambao walijadili makubaliano hayo, watatoa tathmini baadaye katika miezi ijayo kwa mataifa ya EU.