EU-UINGEREZA

Gove kumuunga mkono Johnson kumrithi David Cameron

Kiongozi wa kampeni ya Uingereza kutoka kwenye umoja wa Ulaya, Boris Johnson akizungumza mara baada ya matokeo kutangazwa
Kiongozi wa kampeni ya Uingereza kutoka kwenye umoja wa Ulaya, Boris Johnson akizungumza mara baada ya matokeo kutangazwa REUTERS/Mary Turner/Pool

Waziri wa sheria nchini Uingereza Michael Gove ameweka wazi kuwa atamuunga mkono mwanaharakati kinara wa kambi ya kujiondoa kwenye umoja wa Ulaya Boris Johnson katika jitihada za kuwa waziri mkuu wa Uingereza kuchukua nafasi ya David Cameron aliyetangaza kujiuzulu nafasi hiyo ifikapo mwezi Oktoba kufuatia nchi hiyo kuamua kujiondoa kwenye muungano wa Ulaya. 

Matangazo ya kibiashara

Hapo jana Gove alimpigia simu Boris ambaye ni meya wa zamani wa jijini la London na kumwambia kuwa atasimama naye na kuunda nguvu ya pamoja kwa ajili ya manufaa ya nchi.

Kwa upande mwingine washirika wa karibu wa waziri wa mambo ya ndani Theresa May, jana usiku walikuwa wakiwaomba wabunge kumuunga mkono May ambaye anaonekana kuwa mpinzani mkuu wa Boris na anatarajia kuingia katika kinyang’anyiro hicho mwishoni mwa juma.

Haya yanajiri wakati mataifa yaliyo asisi muungano wa Ulaya EU, yanaitaka Uingereza kuanza kuondoka katika muungano huo haraka iwezekanavyo ili kuiondoa jumuiya hiyo katika mkwamo, waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani amesema jana Jumamosi.

Frank- Walter Steinmeier akiongoza mkutano wa mataifa sita yaliyo asisi Muungano wa Ulaya jijini Berlin, amesema wako katika makubaliano kwamba Uingereza haitakiwi kusubiri utaratibu mgumu wa kujiondoa katika muungano huo.