UTURUKI

Rais Erdogan asema jaribio la mapinduzi limeshindwa

Gari la jeshi jijini Istanbul  wakati wa jaribio la kijeshi
Gari la jeshi jijini Istanbul wakati wa jaribio la kijeshi REUTERS/Baz Ratner

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amelaani jaribio la mapinduzi ya kijeshi dhidi ya serikali yake kusisitiza kuwa bado yupo madarakani.

Matangazo ya kibiashara

Aidha, amesema jaribio hilo lililotekelezwa na kundi la wanajeshi ni la uhaini na watachukuliwa hatua kali.

Kundi hilo la kijeshi kuanzia Ijumaa usiku limekuwa likijaribu kuchukua madaraka baada ya makabiliano makali jijini Ankara, Istanbul na miji mingine.

Kaimu Mkuu wa jeshi Jenerali Umit Dundar ametangaza kuwa watu 104 waliopanga mapinduzi hayo wameuawa huku wengine 1,563 wakikamatwa.

Hadi sasa Mkuu wa Majeshi bado hajaokolewa baada ya kutekwa na kundi hilo la wanajeshi.

Kifaru cha jeshi jijini Ankara
Kifaru cha jeshi jijini Ankara 路透社

Jaribio hili lilianza kushuhudiwa siku ya Ijumaa jioni baada ya kundi hilo la wanajeshi likiwa limejihami kwa silaha nzito na kufunga barabara kuu jijini Instanbul na kupaa angani kutumia ndege za kijeshi.

Baadaye kundi hilo lilitoa taarifa kuwa serikali ya rais Erdogan ilikuwa imepinduliwa na jeshi lilikuwa madarakani.

Maafisa wa polisi wakipiga doria jijini Ankara
Maafisa wa polisi wakipiga doria jijini Ankara REUTERS/Murad Sezer

Wakati wa jaribio hilo, rais Erdogan alikuwa mapumzikoni huko Marmaris na baadaye kuwahotubia raia wa nchi hiyo kuwaomba kujitokeza kupinga jaribio hili.

Mataifa mbalimbali ikiwemo Marekani imelaani jaribio hili na kutaka hali ya kawaida kurejeshwa haraka nchini humo.