UINGEREZA-BREXIT

Mahakama kuu ya London yasema waziri mkuu hana mamlaka kutengua ibara ya 50

Mahakama kuu ya jijini London, Uingereza imetoa uamuzi ikisema kuwa, ni bunge na sio Serikali ndilo linalopaswa kuidhinisha mpango wa nchi hiyo kujiondoa kwenye umoja wa Ulaya, uamuzi ambao sasa huenda ukachelewesha zoezi la nchi hiyo kuanza mchakato wa kujitoa.

Gina Miller, mmoja wa watu ambao walifungua kesi mahakama kuu kupinga tangazo la waziri mkuu Theresa May.
Gina Miller, mmoja wa watu ambao walifungua kesi mahakama kuu kupinga tangazo la waziri mkuu Theresa May. REUTERS/Toby Melville
Matangazo ya kibiashara

Majaji watatu wametoa uamuzi kuwa, waziri mkuu Theresa May hakuwa na haki ya kutumia mamlaka yake kutengua ibara ya 50 ya mkataba wa Lisbon ulioanzisha Jumuiya ya Ulaya.

Uamuzi huu umekuja ikiwa ni miezi michache tu imepita, toka waziri mkuu Theresa May atangaze kuwa nchi yake imeanza mchakato wa kutengua ibara ya 50 ya mkataba wa Lisbon, mchakato utakaoshuhudia nchi hiyo ikijiondoa rasmi kwenye umoja huo ndani ya muda wa miaka miwili.

"Tumeamua kuwa, kisheria waziri mkuu hana madaraka ya kikatiba kutoa agizo la kuanza mchakato wa kutengua ibara ya 50 kwa nchi ya Uingereza kuanza kujiondoa kwenye umoja wa Ulaya," walisema majaji wa mahakama kuu.

Hata hivyo Serikali imepewa nafasi na muda wa kukata rufaa kwenye mahakama ya juu ya nchi.

Waziri wa biashara za kimataifa wa Uingereza, Liam Fox amesema kuwa Serikali "imesikitishwa" na uamuzi wa mahakama kuu, ambapo ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuheshimu maamuzi ya wananchi kupitia kura ya maoni iliyofanyika.

Waziri mkuu May alisema kuwa nchi yake itaanza kutekeleza utenguzi wa ibara ya 50 ifikapo mwishoni mwa mwezi Machi, akiwatuhumu watu waliofungua kesi mahakamani kuwa wanalenga kuchelewesha mchakato wenyewe.

Wajumbe wengi kwenye bunge la walio wengi walipiga kampeni kwa nchi ya Uingereza kusalia kwenye umoja wa Ulaya wakati wa kura ya maoni ya mwezi Juni mwaka huu, ambapo kuna uvumi kuwa huenda wakapendekeza kucheleweshwa kwa mchakato ama kurahisishwa kwa masharti ya nchi hiyo kujitoa.