IRAQ-UN

Mapigano yaendelea Mosul wakati huu kukiripotiwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu

Wanajihadi wa ISIL nchini Iraq wanadaiwa kutekeleza mauaji ya raia
Wanajihadi wa ISIL nchini Iraq wanadaiwa kutekeleza mauaji ya raia

Jeshi la Iraq limekabiliana na wanajihadi wa Islamic State katika mitaa ya Mosul wakati huu umoja wa mataifa ukiripoti kuwa wanajihadi wameendelea kuwachinja watu kadhaa ndani ya mji huo.

Matangazo ya kibiashara

Hayo yanajiri wakati huu Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra ad Al Hussein akitoa wito wa hatua za haraka kuchukuliwa ili kuhakikisha kwamba haki na mahitaji ya waathirika vinazingatiwa ikiwa ni pamoja na kuangalia kiundani, haja ya haki, ukweli na maridhiano nchini Iraq.

Ofisi yake imepokea habari kuhusu makaburi ya pamoja, ushahidi zaidi wa vitendo vya ukatili wa kingono kwa wanawake na wasichana, mateso na mauaji, ajira kwa watoto na ukiukwaji mwingine mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na ISIL nchini Iraq.

Amesema kuna ripoti iliyoibuka ya visa mbalimbali vya mateso dhidi ya raia, akiongeza kuwa picha zinazoonekana ni za kusikitisha, watoto wana lazimishwa kufanya mauaji, wanawake kugawanywa miongoni mwa wapiganaji wa kigaidi wa ISIL na mauaji ya wale wanaodhaniwa kwenda kinyume na mafundishoya ISIL.