UFARANSA-USALAMA

Wanawake kutoka Qatar waibiwa Euro milioni 5 mjini Paris

Moja ya maeneo ya mji mkuu wa Ufaransa, Paris ambako visa vya wizi vimekua sugu.
Moja ya maeneo ya mji mkuu wa Ufaransa, Paris ambako visa vya wizi vimekua sugu. REUTERS/Charles Platiau

Watu wasiojulikana ambao walijificha nyuso zao wamewaibia wanawake wawili kutoka Qatar na dereva wao kwenye barabara kuu kaskazini mwa mji wa Paris, nchini Ufaransa.

Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa vyanzo vya polisi, watu hao waliiba vitu vyenye thamani ya Euro milioni 5.

Wanawake hao walikua wakitokea kwenye uwanja wa ndege wa Bourget wakiwa ndani ya gari lao aina ya Bentley Jumatatu usiku, wakati ambapo walilazimishwa kuondoka barabarani na kurushiwa mabomu ya machozi.

"Kila kitu kilichokua ndani ya gari: vito, mavazi, mizigo vilichukuliwa," chanzo cha polisi kimeliambia shirika la habari la AFP.

Miaka miwili iliyopia, mwanamfalme kutoka nchini Saudi Arabia aliibiwa katika eneo hilo.

Uwanja wa ndege wa Bourget unachukuliwa kama eneo kunakofanyika 'visa mbalimbali barani Ulaya'.

Kim Kardashian pia aliporwa vito vyenye thamani ya Euro milioni 6 katika ghorofa la kifahari la mjini Paris.

Mapema mwezi huu, serikali ya Ufaransa ilitangaza fedha za ziada kwa ajili ya sekta ya utalii, na kuahidi kuweka kamera zaidi za kuwakagua watu mbalimbali katika maeneo ya mji mkuu yanayolengwa na wezi.