UJERUMANI

Mgomo wa marubani wa ndege za Lufhansa wazua kizaazaa Ujerumani

Ndege za Lufthansa zikiwa zimepaki kwenye moja ya uwanja wa ndege wa Ujerumani.
Ndege za Lufthansa zikiwa zimepaki kwenye moja ya uwanja wa ndege wa Ujerumani. REUTERS/Michael Dalder

Shirika la ndege la Ujerumani, Lufthansa, limetangaza kuahirisha safari zake zaidi ya 900, Jumatano Novemba 23, kwa kile shirika hilo limesema ni kwa sababu ya mgomo wa marubani wake, ambapo maelfu ya wasafiri wameathirika. 

Matangazo ya kibiashara

Mgomo huu umetokana na madai ya muda mrefu ya marubani hao kuhusu nyongeza ya mshahara na marupurupu mengine wanayolidai shirika hilo.

Mgomo huu umeitishwa na shirikisho la chama cha marubani, ambapo umeathiri safari za shirika la Lufthansa kwenye maeneo mengi pia ya ndani ya nchi.

Kati ya safari zake 3000 inazofanya, safari 876 zilifutwa kutokana na mgomo huo, ambao unadaiwa kuathiri zaidi ya wasafiri laki 1 wanaotumia shirika hilo kwa usafiri, imesema taarifa ya wakuu wa shirika hilo.

Orodha ya safari za ndege za Lufthansa, ambazo zimeahirishwa kutokana na mgomo.
Orodha ya safari za ndege za Lufthansa, ambazo zimeahirishwa kutokana na mgomo. REUTERS/Kai Pfaffenbach

Marubani hao wametishia kuendelea na mgomo wao hadi siku ya Alhamisi. Huu ukiwa ni mgomo wa 14 kufanywa na wafanyakazi hao toka April mwaka 2014.

Awali mgomo huu ulikuwa uwe wa saa 24, lakini baadae walitangaza kuwa mgomo huo utaendelea hadi siku ya Alhamisi ambapo utahusu pia safari za nje ya Ujerumani za shirika hilo.

Katika hatua nyingine, mgomo mwingine wa wahudumu wa ndege za Lufthansa za gharama za chini, nao umeathiri safari zaidi ya 60.

Mgomo huu umepewa baraka zote na shirikisho la vyama vyama vya wafanyakazi, Verdi kutokana na wakuu wa shirika hilo kushindwa kuwapa marubani hao nyongeza ya mshahara wanaodai.