UKIP-UINGEREZA

Chama kilichoongoza kampeni ya Uingereza kujitoa EU kupata kiongozi mpya

Chama cha upinzani nchini Uingereza UKIP kinachopingana na sera za umoja wa Ulaya, Jumatatu ya wiki ijayo kinatarajiwa kumtangaza kiongozi mpya wa chama hicho kuziba nafasi ya Nigel Farage aliyeongoza kampeni ya nchi yake kujitoa kwenye umoja wa Ulaya.

Aliyekuwa kiongozi wa chama cha UKIP nchini Uingereza, Nigel Farage.
Aliyekuwa kiongozi wa chama cha UKIP nchini Uingereza, Nigel Farage. REUTERS/Suzanne Plunkett
Matangazo ya kibiashara

Licha ya ushindi baada kufanikiwa kuwashawishi wananchi wa Uingereza kupiga kura ya ndio kujitoa umoja wa Ulaya, chama hicho kinakabiliwa na mgawanyiko mkubwa wa ndani ya chama, ambapo viongozi wa juu wa chama hicho wameahidi kumaliza tofauti zao na kuleta umoja.

Toka kujiuzulu nafasi yake baada tu ya kumalizika kwa kura ya maoni kujitoa umoja wa Ulaya mwezi Juni mwaka huu, Farage alipeleka kampeni yake ya mafanikio nchini Marekani, ambako akawa mshirika wa karibu wa rais mteule wa Marekani, Donald Trump.

Lakini chama cha UKIP kimekuwa kikishuhudia mgawanyiko wa ndani, ikiwemo kujiuzulu kwa viongozi wa juu wa chama, kwa madai kuwa kilitumia fedha za umoja wa Ulaya vibaya pamoja na makabiliano ya wenyewe kwa wenyewe kwenye bunge la Ulaya.

Wagombea watatu ndio watakaochuana kuwania nafasi hiyo, yumo naibu kiongozi wa chama Paul Nuttal, aliyewahi kuwa naibu mkuu wa chama, Suzanne Evans na mwanaharakati wa chama John Rees-Evans, huku mshindi akitarajiwa kutangazwa Novemba 28, baada ya kura za wanachama.

Nuttal, mbunge katika bunge la kitaifa na anayepewa nafasi ya kushinda nafasi hiyo, amepa kutengeneza umoja na mshikamano wa chama ikiwa atachaguliwa, akiapa kumaliza mivutano inayoshuhudiwa.

Evans, ripota wa zamani wa shirika la utangaza la Uingereza BBC, anatajwa kuwa mpinzani wake wa karibu sana, ambapo amesema chama chake lazima kipanue wigo wa kujumuisha wanachama wote hasa wanawake na wale waliotengwa.

Upande wa mgombea, Rees-Evans, mwanajeshi wa zamani, yeye amejikuta akikabiliwa na changamoto ya kupata uungaji mkono hasa baada ya kuapa kurejesha adhabu ya kifo.