UFARANSA-SIASA

Rais Hollande atangaza kutowania urais mwaka ujao

Rais wa Ufaransa François Hollande
Rais wa Ufaransa François Hollande Television via REUTERS

Rais wa Ufaransa Francois Hollande ametangaza kuwa hatawania urais kwa muhula wa pili mwaka ujao.

Matangazo ya kibiashara

Hollande mwenye umri wa miaka 62 anakuwa rais wa kwanza wa nchi hiyo kufanya maamuzi hayo baada ya kuongoza kwa muhula mmoja tangu mwaka 2012.

“Nilitaka niliweke hili wazi kama, nilivyowaambia hapo awali, kuwa nitaamua mwezi Desemba na sasa nimeamua kuwa sitawania tena,” amesema Hollande.

Hii inamaana kuwa chama chake cha Socialist kitamtafuta mgombea mwingine, kupambana na mgombea wa chama cha Republican Francois Fillon na Marine Le Pen kutoka chama cha National Front.

Umaarufu wa Hollande umeshuka kutokana na Ufaransa kushambuliwa kigaidi lakini pia serikali yake imekuwa katika mstari wa mbele kutuma wanajeshi kwenda kulinda amani katika nchi mbalimbali kupambana na ugaidi.

“Kama mnavyojua Ufaransa, bara la Ulaya na dunia ilipitia wakati mgumu wa kukabiliana na hali ngumu ya kiusalama,”.

“Niliruhusu wanajeshi wetu kwenda nchini Mali, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Syria na Iraq kwenda kusaidia kulinda amani,” aliongeza Hollande akizungumza Jumatatu usiku.

Wachambuzi wa siasa wanasema hatua ya Hollande umekuja kwa wakati muafaka na ni habari nzuri kwa chama cha Socialist kumtafuta mgombea mwingine.

Hadi kuamua kufikia maamuzi haya, rais Hollande alikuwa amepoteza ushirikiano wa chama chake na wananchi wa Ufaransa wanaolalamikia hali ngumu ya maisha na kiusalama.

Waziri Mkuu Manuel Valls, ambaye anatarajiwa kuwania tiketi ya chama hicho kuwania urais mwakani, amefurahishwa na kupongeza hatua hiyo ya rais Hollande.