ITALIA

Waziri mkuu wa Italia, Matteo Renzi ajiuzulu

Matteo Renzi, waziri mkuu wa Italia, wakati akitangaza kujiuzulu nafasi yake.
Matteo Renzi, waziri mkuu wa Italia, wakati akitangaza kujiuzulu nafasi yake. REUTERS/Tony Gentile

Waziri mkuu wa Italia, Matteo Renzi, ametangaza kujiuzulu nafasi yake, saa chache baada ya kuthibitishwa kuwa, ameshindwa vibaya katika kura ya maoni kuhusu mabadiliko ya katiba.

Matangazo ya kibiashara

Matokeo ya awali yaliyotolewa na wizara ya mambo ya ndani ya nchi, yameonesha kuwa upande wa kambi ya kampeni ya Hapana uliokuwa unaoongozwa na vuguvugu maarufu hivi sasa nchini humo la Five Star, unaelekea kupata ushindi wa asilimia 60 dhidi ya 40 za kambi ya upande wa waziri mkuu Renzi.

Masoko ya hisa yameporomoka asubuhi hii baada yatangazo la Renzi, ambapo biashara kwenye masoko ya hisa barani Ulaya na Asia pamoja na thamani ya euro zimeporomoka maradufu.

Waziri mkuu Renzi amesema siku ya Jumatatu atamtembelea rais Sergio Mattarella kuwasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa mkono, baada ya kukutana na baraza lake la mawaziri.

Kwa mantiki hii ni wazi sasa rais Mattarella anakasimiwa jukumu la kufanya mazungumzo kuunda Serikali ya kitaifa na ikiwa atashindwa atalazimika kuitisha uchaguzi mkuu wa mapema.

Vuguvugu la Five Star lililoundwa na Beppe Grillo, ametaka uchaguzi mwingine ufanyike ndani ya wiki moja ijayo kulinga na sheria mpya za uchaguzi zilizopitishwa hivi karubuni na bunge.

Grillo amesema "demokrasia imeibuka na ushindi" akiandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa Twitter.

Kwa upande wake waziri mkuu Renzi amesema "upande wa kampeni ya Hapana umeshinda kihalali na kwamba ana heshimu maamuzi ya wananchi na anatimiza kile alicho ahidi".