UFARANSA-SIASA

Hollande amteua Bernard Cazeneuve kuwa waziri mkuu mpya

Aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa, Bernard Cazeneuve, ambaye sasa amechaguliwa kuwa waziri mkuu mpya.
Aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa, Bernard Cazeneuve, ambaye sasa amechaguliwa kuwa waziri mkuu mpya. REUTERS/Jacky Naegelen

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa, Bernard Cazeneuve, amechaguliwa kuwa waziri mkuu mpya, akichukua nafasi ya Manuel Valls, aliyetangaza kujiuzulu nafasi yake ili kuwania nafasi ya kuteuliwa na chama chake cha Kisocialist kupeperusha bendera ya urais katika uchaguzi mkuu wa mwakani.

Matangazo ya kibiashara

Cazeneuve, ambaye ameshuhudia na kusimamia masuala ya usalama wakati wa mashambulizi ya wapiganaji wa kijihadi jijini Paris na maeneo mengine ya nchi yaliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 230 katika kipindi cha miaka miwili, atachukua uongozi wa shughuli za Serikali za chama tawala cha Socialist.

Waziri huyu wa ulinzi ameteuliwa kushika nafasi ya waziri mkuu, baada ya rais Francois Hollande, kukubali barua ya kujiuzulu kwa aliyekuwa waziri mkuu wake, Manuel Valls, mapema Jumanne asubuhi, Desemba 6.

Valls, ambaye amekuwa waziri mkuu katika kipindi cha miaka miwili na nusu, Jumatatu ya wiki hii Desemba 5, alitangaza kuwa angeachia nafasi yake ili ajikite katika mbio za kuwania urais kupitia chama chake na kujiandaa na mchujo wa awali mwezi Januari mwakani.

Rais Hollande akiwa na aliyekuwa waziri wake mkuu, Manuel Valls
Rais Hollande akiwa na aliyekuwa waziri wake mkuu, Manuel Valls REUTERS/Philippe Wojazer/File Photo

Katika hotuba yake wakati akitangaza nia ya kuwania urais wa nchi hiyo, Valls, aliapa kupambana vilivyo na vinara wa vyama vya mrengo wa kushoto hasa chama cha National Front cha Marin Le Pen, ambao wanaongoza katika kura ya maoni.

Uamuzi wake umekuja ikiwa ni siku nne zimepita, toka rais Hollande alipoamua kutangaza kuwa, hatowania tena urais kwa muhula wa pili, tangazo lililotoa mwanya kwa Valls kuwania nafasi hiyo.

"Utayari wangu ni sehemu ya maridhiano," Valls, ambaye wakati fulani aliwahi kuwa waziri wa mambo ya ndani, alijinasibu vilivyo katika hotuba yake aliyoitoa nje kidogo ya jiji la Paris, katika mji wa Evry.

Kura za maoni zinaonesha kuwa, Marine Le Pen atashinda au kushika nafasi ya pili katika duru ya kwanza ya uchaguzi lakini atashindwa mbele ya Francois Fillon, mwezi may mwakani.