Hatma ya Uingereza kwa EU kujulikana baada ya kura ya wabunge
Imechapishwa:
Wabunge nchini Uingereza wanapiga kura kuamua mpango wa Waziri Mkuu Theresa May kuanza mchakato wa nchi hiyo kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya mwezi Machi mwaka ujao.
Waziri Mkuu May, ameahidi kuweka wazi mipango yote ya serikali yake kuhusu kujiondoa kwenye umoja huo ikiwa wabunge wataunga mkono mpango wake.
Uongozi wa Umoja wa Ulaya unasema, kwa ratiba ya Uingereza , huenda mambo yote yakakamilika mwaka 2018.
Mahakama kuu ya jijini London, Uingereza imetoa uamuzi ikisema kuwa, ni bunge na sio Serikali ndilo linalopaswa kuidhinisha mpango wa nchi hiyo kujiondoa kwenye umoja wa Ulaya, uamuzi ambao sasa huenda ukachelewesha zoezi la nchi hiyo kuanza mchakato wa kujitoa.
Mapema mwezi Novemba majaji watatu walitoa uamuzi kuwa, Waziri Mkuu Theresa May hakuwa na haki ya kutumia mamlaka yake kutengua ibara ya 50 ya mkataba wa Lisbon ulioanzisha Jumuiya ya Ulaya.
Uamuzi huu ulikuja ikiwa ni miezi michache tu imepita, toka Waziri Mkuu Theresa May atangaze kuwa nchi yake imeanza mchakato wa kutengua ibara ya 50 ya mkataba wa Lisbon, mchakato utakaoshuhudia nchi hiyo ikijiondoa rasmi kwenye umoja huo ndani ya muda wa miaka miwili.