UJERUMANI-IS-USALAMA

Kundi la IS ladai kuhusika na shambulizi katika mji wa Berlin

Shambulizi katika mji wa Berlin, Desemba 19, 2016.
Shambulizi katika mji wa Berlin, Desemba 19, 2016. REUTERS/Pawel Kopczynski

Kundi la Islamic State limedai Jumanne hii jioni kupitia shirika lake la propaganda la Amaq kwamba limehusika na shambulizi la lori dhidi ya soko la kuuza bidhaa za Sikukuu ya Krismasi jijini Berlin na kusababisha vifo vya watu kumi na mbili Jumatatu Desemba 19.

Matangazo ya kibiashara

Awali polisi ya Ujerumani ilitangaza kwamba ilimkamata mtu mmoja, raia wa Pakistan ikimshtumu kuwa miongoni mwa waliohusika na shambulizi hilo. Lakini muda mchache baadaye polisi imesema haina uhakika kuwa raia huyo alihusika na tukio hilo.
Kamanda wa polisi katika mji wa Berlin laus Kandt amesema kuna uwezakano mkubwa sana mshukiwa hajakamatwa.

hayo yanajiri wakati ambapo raia huyo wa Pakistan aliyetuhumiwa kuhusika katika shambulizi mjini Berlin ameachiwa huru.

Kansela Angela Merkel ambaye ametembelea eneo la tukio, amesema itamsikitisha sana ikiwa itabainika kuwa dereva huyo atakuwa ni mkimbizi na kuongeza kuwa ni lazima iaminike kuwa hili ni shambuizi la kigaidi.

Kansela Merkel amekuwa akikosolewa kwa sera yake ya kuwaruhusu wakimbizi kuingia nchini humo kwa hofu za usalama.

Mwaka uliopita, wakimbizi 890,000 wengi kutoka nchini Syria waliruhusiwa kuingia nchini Ujerumani huku wengine 300,000 wakiingia mwaka huu baada ya kukimbia vita.