UJERUMANI-UGAIDI

Polisi nchini Ujerumani wachunguza shambulizi lililotokea sokoni jijini Berlin

Lori lililogonga watu sokoni jijini Berlin nchini Ujerumani
Lori lililogonga watu sokoni jijini Berlin nchini Ujerumani REUTERS/Hannibal Hanschke

Polisi nchini Ujerumani wanachunguza uwezekano kuwa shambulizi lilolotokea katika soko la bidhaa ya Krismasi siku ya Jumatatu, kuwa la kigaidi.

Matangazo ya kibiashara

Dereva wa Lori liliwagonga watu waliokuwa sokoni na kusababisha vifo vya watu 12 na kuwajeuhi wengine 48 huku wanane wakiwa katika hali mahututi.

Ripoti zinasema kuwa, dereva wa Lori hilo amebainika kuwa ni mkimbizi kutoka Pakistan aliyepewa hifadhi nchini humo mwaka uliopita.

Kansela Angela Merkel amesema itamsikitisha sana ikiwa itabainika kuwa dereva huyo atakuwa ni mkimbizi.

“Lazima tudhanie kuwa, hili lilikuwa ni shambulizi la kigaidi,” amesema Merkel.

“Itasikitisha sana ikiwa itabainika kuwa shambulizi hili ni la kigaidi kwa sababu raia wa Ujerumani wamejitolea sana kuwasaidia wakimbizi,”.

“Watakaobainika ni lazima waadhibiwe kwa mujibu wa sheria,” ameongeza Bi. Merkel.

Polisi wamekuwa wakifanya msako katika makaazi moja ya wakimbizi karibu na uwanja wa ndege jijini Berlin, eneo ambalo mshukiwa huyo amekuwa akiishi.

Kansela Merkel amekuwa akikosolewa kwa sera yake ya kuwaruhusu wakimbizi kuingia nchini humo kwa hofu za usalama.

Mwaka uliopita, wakimbizi 890,000 wengi kutoka nchini Syria waliruhusiwa kuingia nchini Ujerumani huku wengine 300,000 wakiingia mwaka huu baada ya kukimbia vita.