UFARANSA-UCHAGUZI 2017

Ufaransa: Wafuasi zaidi wa mgombea urais Francois Fillon waendelea kujiuzulu

Mgombea urais nchini Ufaransa, François Fillon
Mgombea urais nchini Ufaransa, François Fillon GABRIEL BOUYS / AFP

Thierry Solère, kinara aliyeratibu kura za maoni ndani ya chama cha Republican nchini Ufaransa na kisha kuwa msemaji wa mgombea urais wa chama hicho, Francois Fillon, ametangaza kujiuzulu nafasi yake.

Matangazo ya kibiashara

Kujiuzulu kwa Thierry Solère ni mfululizo wa viongozi wa ndani ya chama hicho waliotangaza kujiondoa kwenye kampeni za Fillon baada ya kuibuka kwa tuhuma za ubadhirifu dhidi yake.

Solère, ambaye alimuunga mkono Bruno Le Maire, wakati wa kura za awali za maoni amesema haileti maana yoyote kuendelea kuwa kwenye kampeni za mgombea ambaye anakabiliwa na kashfa kubwa kama hii.

Juma hilo pia, jaji Dominique Bussereau, mmoja kati ya watu waliokuwa wanamuunga mkono Fillon alitangaza nayeye kujiondoa kwenye kambi ya kampeni zake.

Katika hatua nyingine meya wa jiji la Bordeaux, Alain Juppé, ambaye alichuana vikali na Fillon, amesema hatoomba kurejeshwa kwenye nafasi hiyo lakini yuko tayari kusimama kukiwakilisha chama hicho kwenye uchaguzi ujao.

Katika mfululizo wa kudumaza kampeni zake, mhasibu wa kampeni za Fillon, Gilles Boyer, kaimu meneja wake wa kampeni Sebastiba Lecorn na mwakilishi wake wa masuala ya kimataifa, Bruno Le Maire wote kwa pamoja wametangaza kujiondoa kwenye kampeni za Fillon juma hili.