UFARANSA-SIASA

Francois Fillon ajipanga kuingia ikulu licha ya kashfa ya ajira bandia

Francois Fillon, mgombea urais nchini Ufaransa
Francois Fillon, mgombea urais nchini Ufaransa REUTERS/Jean-Paul Pelissier

Mgombea urais nchini Ufaransa Francois Fillon amepambana kuweka matumaini yake hai katika kinyang'anyiro cha urais kabla ya mkutano mkuu wa hadhara leo Jumapili huku mke wake akivunja ukimya wake kuhusu kashfa ya "ajira bandia" ambayo imetishia kutatiza jitihada zake za kuwania urais.

Matangazo ya kibiashara

Fillon ambaye jana Jumamosi alitimiza umri wa miaka 63 , amejaribu kugeuza ukurasa wa juma la jinamizi ambalousaliti wa wafuasi wake baada ya kukiri kwamba atakabiliwa na mashitaka dhidi ya tuhuma za kumpa mkewe kazi bandia katika bunge.

Akizungumza katika mahojiano kwa mara ya kwanza tangu kuibuka kwa shutuma hizo, mke wa Fillon ambaye ni mzaliwa wa Uingereza , Penelope Fillon ameliambia gazeti la Ufaransa kuwa ametekeleza majukumu mbalimbali kwa ajili ya mume wake na kumtaka asonge mbele hadi mwisho.

Tuhuma kwamba Fillon alitoa kazi bandia kwa mkewe Penelope zimegubika juhudi zake za kuwania urais ambapo ameshuhudia waliokuwa wakimuunga mkono wakijitenga naye.

Wakati usaliti ukizidi kuongezeka, wiki saba kabla ya duru ya kwanza ya uchaguzi huo wa hatua mbili utakao fanyika Aprili 23, mwanasiasa mkongwe Allain Juppe mwenye umri wa miaka 71 amesema yuko tayari kuchukua nafasi kama mpeperusha bendera wa chama cha Republican.