EU-UHAMIAJI

Mahakama ya Ulaya yaruhusu nchi wanachama kuwazuia kwa muda wahamiaji

Sehemu ya wahamiaji ambao wameokolewa kutoka kwenye bahari ya Mediterania
Sehemu ya wahamiaji ambao wameokolewa kutoka kwenye bahari ya Mediterania REUTERS/Jon Nazca

Mahakama ya juu ya Umoja wa Ulaya, imesema nchi wanachama zinaweza kukataa kwa muda kutoa viza ya kibinadamu kwa watu ambao wanajaribu kuingia kuomba hifadhi, uamuzi ambao unalenga familia zinazotoka nchini Syria kuingia Ubelgiji.

Matangazo ya kibiashara

Uamuzi wa mahakama ya Ulaya iliyoko mjini Luxembourg, umekuwa ni kama jaribio kwa nchi za Ulaya ambazo zinakabiliwa na wimbi kubwa la wahamiaji katika kipindi cha miaka 2 iliyopita, wengi kutoka nchini Syria.

Katika uamuzi wa kushtua, mahakama imeamua dhidi ya familia zilizotoka kwenye mji wenye vita wa Aleppo nchini Syria na ambao waliomba viza za kibinadamu kuingia Ubelgiji kupitia ubalozi wa nchi hiyo nchini Lebanon.

"Ndio tumeshinda!" amesema waziri wa anayehusika na wahamiaji Theo Francken kupitia mtandao wake wa kijamii wa Twitter.

Mahakama imetoa uamuzi ambao umeenda kinyume na mapendekezo ya mwendesha mashtaka wake aliyesema kukataliwa viza kwa familia hizo kunawaweka hatarini dhidi ya vitendo vya unyanyasaji ikiwa watabakia nchini mwao.