TWITTER-UTURUKI

Akaunti ya Twitter yadukuliwa na maharamia wa mtandao kutoka Uturuki

Anuani kadhaa za mtandao wa Twitter, ikiwemo ile ya klabu ya mpira wa miguu nchini Ujerumani, wizara za Ufaransa na ile ya chaneli ya BBC Amerika Kaskazini, zimefanyiwa udukuzi na maharamia wa mtandao ambao ni wafuasi wa Serikali ya Uturuki walioweka ujumbe wa kukashifu Utawala wa Kinazi wa Ujerumani na ule wa Uholanzi.

Moja ya akaunti ya twitter ya wizara ya uchumi ya Ufaransa iliyovamiwa na maharamia wa mtandao
Moja ya akaunti ya twitter ya wizara ya uchumi ya Ufaransa iliyovamiwa na maharamia wa mtandao Screenshot
Matangazo ya kibiashara

"#NaziGermany, #NaziHolland, huu ni ujumbe mdogo kutoka kwa utawala wa #Ottoman kwaajili yenu na tuonane tarehe 16 April, nataka nini? Nataka mjidunze Kituruki," ulisomeka ujumbe huo, unaoteolewa wakati huu ambapo kuna mzozo mkubwa kati ya nchi za Ulaya na Serikali ya Uturuki.

Ujumbe huo pia ulijumuisha ujumbe wenye nembo ya Swastika uliofuatiwa na picha ya video ikionesha hotuba ya rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan.

Wamiliki wa mtandao wa Twitter wamekiri akaunti yao kushambuliwa na maharamia wa mtandao.

"Tunafahamu kuhusu akaunti kadhaa zilizodukuliwa asubuhi ya leo," amesema msemaji wa mtandao wa Twitter, akiongeza kuwa chanzo cha mashambulizi hayo kimebainika kutoka kwenye program ya nje, ambayo ruhusa yake imeondolewa.

Twitter inasema mfumo wake wa takwimu uliingiliwa na maharamia hao kutumia kama ruta kuvamia akaunti za watu wengine.

"Tayari tumeanzisha uchunguzi kuhusiana na tukio hili," amesema mkurugenzi mtendaji wa Twitter Omer Ginor.

Wizara ya uchumi ya Ufaransa imethibitisha kuwa akaunti yake ilidukuliwa lakini tatizo hilo limeshatatuliwa.

Chaneli ya BBC Amerika Kaskazini iliandika kwenye mtandao wake kuwa, "Kwa muda tumepoteza umiliki wa akaunti yetu ya Twitter lakini shughuli za kawaida zimerejea".

Klabu ya Ujerumani, Borussia Dortmund, mchezaji tenesi wa zamani Boris Becker na akaunti ya Amnesty International pia zilivamiwa na maharamia hao.

Shambulio hili la kimtandao limejiri baada ya wanasiasa wa Uturuki juma lililopita kukataliwa kufanya mikutano nchini Uholanzi na kwenye miji kadhaa ya Ujerumani, ambapo walitaka kuzungumza na waturuki wanaoishi nje ya nchi kuwashawishi kuhusu kura ya maoni ya marekebisho ya katiba.