UINGEREZA

Watu saba wakamatwa kuhusiana na uvamizi wa kigaidi jijini London

Shambulizi jijini London
Shambulizi jijini London Reuters

Watu saba wamekamatwa na Polisi nchini Uingereza kwa tuhma za kuhusika na shambulizi la kigaidi  nje ya bunge la nchi hiyo jijini London siku ya Jumatano.

Matangazo ya kibiashara

Polisi wanasema washukiwa hao wamekamatwa jijini London na mjini Birmingham, huku idadi ya watu waliopoteza maisha ikiwa wanne wala sio watano kama ilivyotangazwa hapo awali.

Miongoni mwa watu waliopoteza maisha ni afisa wa polisi aliyedungwa kisu, lakini pia  raia wengine wa kawaida waliojipata katika eneo la tukio hilo katika eneo la Westminister na kugongwa na gari.

Zaidi ya watu 20 waliojeruhiwa baada ya kugongwa na gari na wengine  kukanyagana, wameendelea kupata matibabu katika hospitali mbalimbali jijini London.

Kuhusu aliyetekeleza uvamizi huo ambao Uingereza imesema ni wa kigaidi, aliuawa pia baada ya kupigwa risasi na afisa wa polisi.

Waziri wa Uingereza Bi.Theresa May amelaani shambulizi hilo matamshi ambayo pia yametolewa na viongozi wengine wa dunia.