UFARANSA-URUSI

Le Pen akutana na rais wa Urusi Vladimir Putin jijini Moscow

Mgombea wa urais nchini Ufaransa kupitia chama cha mrengo wa Kulia cha FNL Marine Le Pen, amekutana na rais wa Urusi Vladimir Putin jijini Moscow.

Mgombea wa urais nchini Ufaransa Marine Le Pen (Kushoto) akisalimiana na rais wa Urusi Vladimir Putin katika Ikulu ya Kremlin jijini Moscow Machi 24 2017
Mgombea wa urais nchini Ufaransa Marine Le Pen (Kushoto) akisalimiana na rais wa Urusi Vladimir Putin katika Ikulu ya Kremlin jijini Moscow Machi 24 2017 Mikhail KLIMENTYEV/SPUTNIK/AFP
Matangazo ya kibiashara

Ikulu ya Moscow imesema kuwa haijaona tatizo la mwanasiasa huyo anayetaka kuwa rais wa Ufaransa kukutana na kiongozi wa nchi hiyo lakini pia wanasiasa wengine wa upinzani.

Haikuwekwa wazi kilichojadiliwa kati ya rais Putin na mgeni wake, lakini wachambuzi wa siasa wanasema kuwa ziara hii inaonesha wazi kuwa Moscow inamuunga mkono.

“Le Pen kukutana na rais Putin na viongozi wa upinzani ni jambo la kawaida kabisa,” amesema msemaji wa Ikulu Dmitry Peskov.

Le Pen ametaka ushirikiano wa karibu na kati ya nchi yake na Urusi katika vita dhidi ya ugaidi.

Awali, alikutana na wabunge nchini Urusi na kuahidi kuwa ikiwa atashinda Uchaguzi wa urais mwezi ujao, ataimarisha zaidi ushirikiano kati ya nchi yake na Urusi.

“Ninapendelea kuimarisha zaidi uhusiano na Urusi, kwa sababu tuna historia ndefu ya ushirikiano,” amemwambia Spika wa bunge Vyacheslav Volodin.

Tangu kuwasili kwake jijini Moscow, Le Pen amekuwa akiripotiwa sana na vyombo vya Habari nchini humo.

Anaelezwa kuwa mwanasiasa aliye na uhusiano wa karibu na Urusi.

Mwaka 2014 chama chake kilipokea mkopo wa Dola Milioni 9.7 kutoka kwa Benki moja ambayo baadaye ilifilisika.