LIBYA-WAHAMIAJI-USALAMA

Wahamiaji waendelea kupoteza maisha katika Mediterranean

Maiti ya mhamiaji katika pwani ya Libya, Machi 23, 2017.
Maiti ya mhamiaji katika pwani ya Libya, Machi 23, 2017. REUTERS/Yannis Behrakis

Miili ya watu waliokufa maji ambayo imeendelea kugunduliwa katika bahari ya Mediterranian inaonyesha kuwa huenda kukawa na watu zaidi waliokufa maji hivi karibuni wakijaribu kusafiri kuelekea Ulaya.

Matangazo ya kibiashara

Siku ya Alhamisi meli ya timu ya waokoaji ya Uhispania iligundua kwenye pwani ya Libya miili 5 ya wahamiaji wa Kiafrika waliokufa maji. Timu ya waokoaji ya Uhispania ina hofu kuwa huenda mamia kadhaa ya watu walikufa maji baada ya meli waliokuemo kuzama katika bahari Mediterranean.

Miili 5 ya vijana, wenye umri kati ya miaka 16 na 25 ambao wanaonekana walikufa maji baada ya boti waliokuemo kuzama, iligunduliwa siku ya Alhamisi mchana na meli ya timu ya waokoaji ya shirika la Uhispania la Proactiva Open Arms, kilomita 21 kutoka pwani ya Libya, nje ya mji wa Sabratha. Miili hiyo ilikua karibu na boti mbili waliokua wakisafiri nazo ambapo inakadiriwa kuwa huenda kati ya watu 240 na 300 walikua wakisafiri na boti hilo, na huenda walikufa maji.

Hii si mara ya kwanza boti kukutwa tupu kupatikana katika pwani ya Libya. Baadhi ya boti zilitoweka, na hali hiyo inaonyesha kuwa idadi ya vifo katika bahari ya Mediterranean inaweza kuwa juu zaidi ya idadi ya watu 5000 iliyotolewa mwaka 2016.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Meli za mashirika ya kibinadamu ziliwaokoa zaidi ya watu 1,000 katika eneo hilo.