UFARANSA

Hollande: Kazi yangu ya mwisho madarakani ni kuzuia chama kama cha Marine Le Pen

Rais wa Ufaransa Francois Hollande akizungumza kwenye mkutano nchini Singapore. Machi 27, 2017
Rais wa Ufaransa Francois Hollande akizungumza kwenye mkutano nchini Singapore. Machi 27, 2017 REUTERS/Edgar Su

Rais wa Ufaransa Francois Hollande amesema kuwa kazi yake ya mwisho wakati anapoelekea kumaliza muhula wake ofisini ni kuhakikisha vyama vyenye umaarufu na vinavyopigania uzalendo na misimamo mikali, havishindi kuingia ikulu na hasa nchini mwake.

Matangazo ya kibiashara

Muhula wa rais Hollande unamalizika kati kati ya mwezi Mei mwaka huu na mwanasiasa kutoka mrengo wa kulia Marine Le Pen anaonekana kuongoza kwenye kura za maoni kuelekea kwenye uchaguzi wamwaka huu wa Ufaransa.

Kauli ya Hollande anaitoa wakati huu nchi ya Uingereza ikitarajia kuanza mchakato wa kujiondoa rasmi kwenye umoja wa Ulaya huku nchi ya Marekani ikiwa imemchagua Donald Trump kama rais, kiongozi anayeonekana kuwa na misimamo mikali.

“Bado nina kazi kubwa ya kufanya kabla sijamaliza muhula wangu na kazi hiyo ni kuhakikisha vyama hivi haviingii madarakani.” alisema rais Hollande wakati akihutubia mkutano nchini Singapore.

Rais Hollande ameanza ziara yake ya mwisho nje ya nchi yake akiwa kama rais, ambapo akitoka nchini Singapore ataelekea nchini Malaysia na baadae Indonesia.

Rais Hollande ameongeza kuwa jukumu la kuhakikisha vyama vyenye misimamo mikali haviingii madarakani sio jukumu la rais peke yake lakini ni jukumu pia la mwananchi.

Uchaguzi wa mwaka huu nchini Ufaransa unatazamwa kwa karibu na mataifa ya Ulaya hasa ambayo yana hofu kuwa huenda vyama vyenye misimamo mikali vikaingia madarakani na kutishia ustawi wa jumuiya ya umoja wa Ulaya.