UJERUMANI-SARAFU YA DHAHABU

Sarafu ya dhahabu yaibiwa Ujerumani Polisi washangazwa namna ilivyoibiwa

Mfano wa sarafu inayofanana na hii ambayo iliibiwa kwenye nyumba ya makumbusho Ujerumani.
Mfano wa sarafu inayofanana na hii ambayo iliibiwa kwenye nyumba ya makumbusho Ujerumani. REUTERS/Heinz-Peter Bader/File Photo

Sarafu kubwa ya dhahabu yenye picha ya Malkia Elizabeth wa pili wa Uingereza inayokadiriwa kuwa na thamani ya dola za Marekani milioni 4, imeibiwa kutoka kwenye jumba moja la makumbusho nchini Ujerumani.

Matangazo ya kibiashara

Sarafu hiyo ya Canada, imepewa jina la “big maple leaf” inaelezwa kuwa thamani yake huenda ikawa kubwa zaidi kutokana na ukweli kuwa sehemu kubwa ya sarafu hiyo ni dhahabu halisi inayofikia kilo 100.

Sarafu hiyo inadaiwa kuibiwa kutoka kwenye jumba la makumbusho la Bode mjini Berlin.
Mpaka sasa haijafahamika ni namna gani wezi hao walifanikiwa kuingia bila kugundulika na mitambo maalumu au waliwezaje kubeba sarafu hiyo yenye ukubwa wa mita 20 na kuondoka nayo bila kubainika.

Kwa mujibu wa vyombo vya usalama mjini Berlin vinasema kuwa huenda dhahabu hiyo ikawa iliibiwa majira saa tisa usiku kwa saa za Ujerumano usiku wa leo.

Sarafu hiyo sio rahisi kubebwa na mtu mmoja na polisi kwenye mji wa Berlin wanaamini kuwa wezi hao waliibeba kupitia dirishani.

Ngazi inayodaiwa kuwa ilitumika ilipatikana ikiwa nyuma ya uzio wa jengo hilo.

“Kulingana na taarifa ambazo tunazo kwa sasa ni kuwa wezi hao walivunja kioo kwa nyuma ya makumbusho iliyo jirani na reli,” amesema msemaji wa Winfrid Wenzel.

Polisi wanasema sarafu hiyo ilikuwa imehifadhiwa kwenye glasi maalumu isiyoingiza risasi ndani ya jengo hilo. Hata hivyo Polisi imekataa kutoa taarifa zaidi kuhusiana na tukio hilo.

Sarafu hiyo ilitengenezwa na Kasri la kifalme la Canada mwaka 2007.

Sarafu hiyo ina unene wa sentimita 3 na kipenyo cha sentimita 53 ambapo ina sura ya malkia Elizabeth wa pili upande mmoja na mwingine ina sura ya kiongozi wa Serikali ya Canada.