UFARANSA-CHINA

Vurugu zimezuka jijini Paris baada ya kuuawa kwa raia wa China

Kumetokea vurugu kubwa jijini Paris Ufaransa baada ya kuuawa kwa raia mmoja wa China, ambapo Polisi watatu wamejeruhiwa na mamia ya watu wamekamatwa kuhusiana na vurugu hizo.

The scene in Paris's 19th arrondissement on Monday night
The scene in Paris's 19th arrondissement on Monday night Zeenat Hansrod/RFI
Matangazo ya kibiashara

Waandamanaji walikusanyika nje ya kituo kikuu cha Polisi jijini Paris kutoa heshima zao za mwisho kwa raia huyo wa China aliyeuawa.

Familia ya raia huyo imekanusha taarifa ya Polisi kuwa mtoto wao alimshambulia afisa wa Polisi kwa kitu chenye ncha kali wakati walipofika kutatua mzozo wa kifamilia kwenye nyumba yake.

Tayari nchi ya China imetoa taarifa kuhusiana na tukio hili na kuitaka Serikali ya Ufaransa kutoa usalama kwa raia wake.

Liu Shaoyo mwenye umri wa miaka 56 na baba wa watoto watano, aliuawa kwa kupigwa risasi usiku wa Jumapili kwenye kitongoji cha Arrondissement.

Polisi wanasema raia huyo alimshambulia afisa wa Polisi punde tu baada ya kutokea mlangoni na kwamba Polisi aliyeenda alinusurika kwakuwa alikuwa amevaa vesti ya kuzuia risasi.

Hata hivyo wakili wa familia yake amesema wanapinga kabisa taarifa hiyo ya polisi.

Mmoja wa watoto wake alipohojiwa na kituo kimoja cha televisheni, alisema baba yake alikuwa ameshika mkasi aliokuwa anautumia kutengenezea samaki.

Mtoto huyo ameongeza kuwa Polisi walitumia nguvu kuingia ndani ya nyumba yao na kwamba risasi ilifyatuka na kumlenga baba yao.

Wizara ya mambo ya nje ya China tayari imeandika barua kwa mamlaka nchini Ufaransa kutoa maelezo ya kina kuhusiana na tukio hilo na kutaka raia wake kulindwa.

Kamati maalumu ya kukagua Polisi inatarajiwa kwenda kuwaoji wanafamilia wake.

Watu zaidi ya 35 wameripitiwa kushikiliwa na Polisi kwenye maandamano ambayo watu zaidi ya 150 walishiriki.

Polisi nchini Ufaransa wanatuhumiwa kwa kutumia nguvu kubwa sana dhidi ya waandamanaji pamoja na kuwadhalilisha watuhumiwa.