UINGEREZA-EU

Uingereza imeanza rasmi kujitoa kwenye umoja wa Ulaya

Rais wa tume ya umoja wa Ulaya, Donald Tusk, akipokea barua rasmi kumtaarifu Uingereza kuanza kutoka kwenye umoja wa Ulaya. Machi 29, 2017
Rais wa tume ya umoja wa Ulaya, Donald Tusk, akipokea barua rasmi kumtaarifu Uingereza kuanza kutoka kwenye umoja wa Ulaya. Machi 29, 2017 REUTERS/Yves Herman

Hatimaye Uingereza imeanza rasmi mchakato wa kutoka kwenye Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, ikisema “hakuna kurudi nyuma” kutokana na uamuzi ambao umeigawa nchi hiyo na kuibua maswali mengi kuhusu mustakabali wa jumuiya hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Ikiwa ni siku chache tu toka jumuiya hiyo iadhimishe miaka 60 ya uwepo wake, Uingereza imekuwa nchi ya kwanza kuondoka kwenye jumuiya ya nchi 28 wanachama, ikitoa pigo kwenye moyo wa ushirikiano wake toka kumalizika kwa vita kuu ya pili ya dunia.

“Hii ni hatua ya kihistoria ambayo kamwe hakuna kurudi nyuma,” amesema waziri mkuu Theresa May wakati akiwahutubia wabunge Jumatano hii.

Miezi 9 baada ya hatua ya kushangaza ya Uingereza kupiga kura kujiondoa kwenye umoja wa Ulaya, nchi hiyo imeanza kutekeleza hatua ya awali ya kutengua ibara ya 50 ya mkataba wa Lisbon, ikianza kuhesabu muda wa miaka miwili hadi kutamatisha utaratibu wa kuwa imejiondoa kabisa.

“Tayari tumewamisi,” amesema rais wa tume ya Ulaya Donald Tusk mjini Brussels baada ya kupokea barua rasmi kumtaarifu nia ya Uingereza kujitoa.

Waziri mkuu wa Uingereza, Theresa May. 29 Machi, 2017
Waziri mkuu wa Uingereza, Theresa May. 29 Machi, 2017 Parliament TV handout via REUTERS

Hata hivyo rais wa Ufaransa ameonya kuwa kujiondoa kwa Uingereza kutakuwa na maumivu makali kwa Waingereza.

Umoja wa Ulaya umesisitiza kulinda umoja wake ambapo umeongeza kuwa kujitoa kwa Uingereza hakutashawishi nchi zaid kujiondoa.

Barua ya kurasa sita iliyotiwa saini na waziri mkuu May na kuwasilishwa kwa mkono na balozi wake kwenye umoja huo Tim Barrow jijini Brussels, imetaka kuheshimiwa na kuwa na ushirikiano wa heshima kati yao.

May kwenye barua yake amesisitiza umuhimu wa kushirikiana kwenye masuala ya usalama, akisema kushindwa kufikia makubaliano katika hili kutamaanisha kuwa ushirikiano kwenye vita dhidi ya ugaidi utadhoofika.

Waziri mkuu May amesisitiza nia yake ya kuanzisha ushirikiano mpya na umoja wa Ulaya katika kipindi cha miaka miwili ijayo.