UFARANSA-SIASA

Asilimia 70 ya Wafaransa wasema rais Hollande amekuwa rais mbaya

Rais wa Ufaransa Francois Hollande
Rais wa Ufaransa Francois Hollande Reuters

Asilimia 70 ya raia wa Ufaransa wanaamini kuwa rais Francois Hollande hajaongoza vizuri kwa muda wa miaka mitano aliyokuwa madarakani, na hivyo amekuwa rais mbaya.

Matangazo ya kibiashara

Hili limebainika baada ya kutolewa kwa matokeo ya kura ya maoni dhidi ya kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 62 ambaye hatawania tena urais.

Shirika  la Odoxo lililoongoza kura hiyo ya maoni limesema kuna asilimia ndogo ya raia wa nchi hiyo wanaona kuwa ataacha rekodi nzuri.

Asilimia 54 ya waliohojiwa wameonekana kupendezwa na namna alivyoshughulikia maswala ya usalama na ndoa kati ya watu wa jinsia moja.

Kuhusu uchumi,  ni asilimia 16 ya raia wa Ufaransa waliosema kuwa wameridhika na rekodi yake.

Kura hii ya maoni imekuja wakati huu Ufaransa ikielekea kwenye Uchaguzi Mkuu tarehe 23 mwezi Aprili.

Wachambuzi wa siasa nchini humo wanaona kuwa ushindani mkali unatarajiwa kuwa kati ya Emmanuel Macron, Marine Le Pen kutoka chama cha mrengo wa kushoto na mgombea wa Republican Francois Fillon.

Wagombea wengine nane, wanawania urais.

Watakaomaliza katika nafasi ya kwanza na ya pili, watamenyana katika mzunguko wa pili.