UCHAGUZI UFARANSA 2017

Wagombea urais Ufaransa kutamatisha kampeni zao

France-présidentielle 2017: affiches des deux candidats finalistes
France-présidentielle 2017: affiches des deux candidats finalistes REUTERS/Eric Gaillard

Wagombea wawili nchini Ufaransa ambao wanawania kuwa rais ajae wa taifa hilo Ijumaa hii wanafanya kampeni zao kuwashawishi wapiga kura kuwachagua wakati wa duru ya pili siku ya Jumapili, May 7.

Matangazo ya kibiashara

Mgombea Emmanuel Macron ambaye anapewa nafasi ya kushinda kinyang’anyiro cha siku ya Jumapili, yuko kusini mwa mji wa Rodez kuongea na wapiga kura wapya.
Mpinzani wake Marine Le Pen hapo jana alijikuta pabaya baada ya kurushiwa mayai wakati akifanya kampeni kwenye mji wa Brittany.

Wakati huohuo mgombea Emmanuel Macron amefungua kesi mahakamani kuhusiana na uvumi ulioenea mtandaoni kuwa anamiliki akaunti kwenye benki moja iliyoko kwenye visiwa vya Caribbean.

Macron amekanusha vikali tuhuma dhidi yake ambazo zilielezwa na mpinzani wake Le Pen wakati wa mjadala wao wa mwisho wa televisheni siku ya Jumatano.

Kura ya maoni iliyofanywa na taasisi ya Odoxa ya nchini Ufaransa imetabiri kuwa kutakuwa na idadi ndogo ya wapiga kura watakaojitokeza kwenye uchaguzu wa Jumapili hali ambayo haijawahi kushuhudiwa toka mwaka 1969.

Kura hiyo imetabiri pia wapiga kura wa mrengo wa kushoto huenda wasipige kura.

Kura nyingine tofauti iliyofanywa na Elabe kwa BFMTV na L’Express, imeonesha kuwa uungaji mkono wa mgombea Emmanuel Macron umeongezeka kwa asilimia 62 huku mpinzani wake akiwa na asilimia 38.