Marine Le Pen akubali kushindwa, asema Wafaransa wamekataa kuchagua mabadiliko
Imechapishwa:
Aliyekuwa mgombea wa urais nchini Ufaransa Bi. Marine Le Pen amekubali kushindwa katika duru ya pili ya Uchaguzi wa urais uliofanyika siku ya Jumapili.
Akizungumza na wafuasi wake punde tu baada ya matokeo ya awali kutolewa, yalionesha kuwa mpinzani wake Emmanuel Macron amemshinda kwa kupata asilimia 65.1 ya kura, Marine aliyepata asilimia 34.9 amesema raia wa Ufaransa wameamua kuendelea na uongozi uliopo.
"Raia wa Ufaransa wameamua kuendelea na uongozi uliozoeleka, hawakuchagua mabadiliko," aliongeza Le Pen.
“Nimezungumza na Macron na kumpongeza kwa ushindi, namtakia kila la heri katika kutekeleza majukumu mazito yaliyo mbele yake,” aliongeza Le Pen.
Aidha amesema kuwa sasa ataendeleza siasa za upinzani baada ya kumalizika kwa uchaguzi huouliokuwa na ushindani mkali.
Imekuwa ni mara ya pili kwa mwanasiasa huyu anayeongoza chama cha mrengo wa kulia cha Front Nationale kuwania urais nchini Ufaransa bila mafanikio.
Mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 2012 na sasa mwaka 2017.