UCHAGUZI UFARANSA 2017

Raia wa Ufaransa wamchagua Emmanuel Macron kuwa rais mpya wa Jamhuri

Emmanuel Macron, rais mpya wa Ufaransa
Emmanuel Macron, rais mpya wa Ufaransa Ảnh FMM

Matokeo ya awali yameanza kutangazwa nchini Ufaransa ambapo kwa mujibu wa matokeo yaliyotolewa na wizara ya mambo ya ndani ya Ufaransa yanaonesha mgombea Emmanuel Macron anaongoza kwa asilimia 65.1 dhidi ya asilimia 34.9 aliyopata Marine Le Pen.

Matangazo ya kibiashara

Muda mfupi uliopita Marine Le Pen amewahutubia wafuasi wake na kutangaza kumpongeza Macron kwa ushindi alioupata huku akisema uchaguzi huu umekuwa ni wa kihistoria.

Le Pen amesema matokeo haya yametoa taswira mpya kwa siasa za Ufaransa ambapo amewashukuru wapiga kura wake kwa kumuunga mkono toka kwenye duru ya kwanza ya uchaguzi.

Kiongozi huyo ameongeza kuwa yeye ataongoza upinzani bungeni ili katika kuhakikisha nchi yao inarejea kwenye ramani ya dunia.

Taarifa za ndani zinasema kuwa Macron pia alimpigia Marine Le Pen na kumpongeza kwa upinzani aliouonesha wakati wa kipindi chote cha kampeni.

Ushindi wake unamaliza miezi kadhaa ya hofu waliyokuwa nayo viongozi wa jumuiya ya Ulaya ikiwa mgombea Marine Le Pen angeshinda kwenye kinyang’anyiro cha mwaka huu.

Viongozi mbalimbali wa dunia wameendelea kutuma salamu za pongeza kwa raia wa Ufaransa na Emmanuel Macron wakimpongeza kwa ushindi wake waliosema ni wa kishindo.

Rais wa Ufaransa anayemaliza muda wake Francois Hollande amempongeza Macron kwa ushindi wake na kumtakia kheri.

Kansela wa Ujerumani na rais wa tume ya umoja wa Ulaya Jean Claude Junker nao wametuma salamu za pongezi kwa Macron wakiwashukuru wananchi wa Ufaransa kwa kufanya maamuzi sahihi ya kumchagua mpenda mabadiliko na kiongozi anayeona Ulaya mpya.