UFARANSA-SIASA

Wasifu wa mwanasiasa Marine Le Pen

Mwanasiasa wa Ufaransa Marine Le Pen aliyegombea urais nchini Ufaransa
Mwanasiasa wa Ufaransa Marine Le Pen aliyegombea urais nchini Ufaransa REUTERS/Charles Platiau

Marion Anne Perrine maarufu kwa jina la "Marine" Le Pen ni mwanasiasa na wakili mwenye umri wa miaka 48.

Matangazo ya kibiashara

Ni mama wa watoto watatu. Baada ya kuachana na wanaume wawili katika mahusiano yaliyopita kwa sasa ameingia katika ndoa ya mkataba.

Baada ya kuibuka wa pili katika mzunguko wa kwanza wa Uchaguzi Mkuu mwezi Aprili, aliamua kujiuzulu kama rais wa chama chake cha National Front, FN kinachoegemea mrengo wa kulia.

Ni binti wa mwisho wa mwanzilishi wa chama hicho FN Jean Marie ambaye alistaafu urais wa chama hicho mwaka 2011, baada ya kukosa urais mwaka 2002.

Hadi kuelekea katika Uchaguzi wa mwaka 2017, Le Pen amekuwa mbunge wa bunge la Umoja wa Ulaya tangu mwaka 2009.

Mara yake ya kwanza kuwania urais nchini Ufaransa ililiwa ni mwaka 2012. Wakati huo alimaliza katika nafasi ya tatu baada ya kupata asilimia 17.90 nyuma ya Francois Hollande na mshindi Nicolas Sarkozy.

Mwaka 2017 ilikuwa ni mara yake ya pili kutafuta uongozi wa Ufaransa na kuwa mmoja wa wagombea waliopewa nafasi kubwa ya kushinda, lakini baada ya mzunguko wa kwanza, alimaliza katika nafasi ya pili kwa asilimia 21.30 nyuma ya mshindi Emmanuel Macron aliyepata asilimia 23.9.

Marine Le Pen mwanasiasa wa Ufaransa aliyegombea urais mwaka 2017
Marine Le Pen mwanasiasa wa Ufaransa aliyegombea urais mwaka 2017

Mwanasiasa huyu amekuwa akisema uongozi wake ni kurejesha tamaduni za Ufaransa, na kufanya Ufaransa kuwa ya Wafaransa kwanza, akiiga mfano wa rais wa Marekani Donald Trump.

Baadhi za ahadi zake zilikuwa ni kuitisha kura ya maoni ili Ufaransa ijiondoe kwenye Umoja wa Ulaya kama Uingereza ilivyofanya.

Pamoja na hilo, aliahidi kuwa uongozi wake ungeachana na sarafu ya Euro inayotumiwa na mataifa ya Ulaya na kurejea katika matumizi ya Franc.

Le Pen pia aliahidi kuwa akiingia madarakani, atapunguza idadi ya wakimbizi 10,000 kila mwaka, kupunguza umri wa kustaafu.

Kuhusu usalama, Le Pen aliahidi kuanzisha mbinu mpya za kukabiliana na wanajihadi ambao wamekuwa wakishtumiwa kutekeleza mashambulizi ya kigaidi nchini Ufaransa.

Sera za Le Pen, zilionekana kuungwa mkono na asilimia zaidi ya 20 ya wpaiga kura nchini humo huku wengine wakimpinga na kumwita mbaguzi.

Rais anayeondoka madarakani Francois Hollande aliwaomba raia wa nchi hiyo kumtompigia kura Marine Le Pen.

Ikiwa angechaguliwa, angekuwa rais wa kwanza mwanamke nchini Ufaransa.