UFARANSA-UJERUMANI-USHIRIKIANO

Hollande azuru Ujerumani kabla ya kukabidhi madaraka kwa Macron

François Hollande na Emmanuel Macron, Juni 16, katika Ikulu ya Elysée.
François Hollande na Emmanuel Macron, Juni 16, katika Ikulu ya Elysée. AFP PHOTO / LIONEL BONAVENTURE

Rais wa Ufaransa anayemaliza muda wake Francois Hollande amefanya ziara yake ya mwisho nchini Ujerumani ambako amekutana na kansela Angela Merkel, ikiwa ni siku chache kabla ya kukabidhi madaraka kwa rais mteule Emmanuel Macron.

Matangazo ya kibiashara

Siku ya Jumatatu kabla ya kuelekea Ujerumani, rais Hollande alikuwa pamoja na Macron wakati wa sherehe za maadhimisho ya kumbukumbu ya vita vya pili vya dunia, ambapo alimpongeza kwa ushindi wake na kueleza historia iliyopo ya kukabidhiana madaraka kwa amani.

Katika hatua nyingine viongozi mbalimbali kutoka barani Afrika wameendelea kutuma salaam za pongezi kwa Macron, ambapo rais wa umoja wa Afrika rais wa Guinea Alpha Conde, amesema ana imani kiongozi huyo ana dira nzuri na bara la Afrika na kwamba ushindi wake ni historia mpya kwa taifa hilo na bara la Afrika.

Akiwa nchini Ujerumani Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema amekuwa mwenye furaha mara zote anapofanya kazi na Hollande na kwamba hivi karibuni atakutana na rais mteule Emmanuel Macron.

Rais anayemaliza muda wake François Hollande na Rais mteule Emmanuel Macron wakati wa hafla ya 8-Mei mjini Paris.
Rais anayemaliza muda wake François Hollande na Rais mteule Emmanuel Macron wakati wa hafla ya 8-Mei mjini Paris. REUTERS/Stephane De Sakutin