Rais Macron achelewesha hatua ya kulitaja Baraza lake la Mawaziri
Imechapishwa:
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameahirisha hatua ya kulitaja Baraza lake la kwanza la Mawaziri hadi siku ya Jumatano.
Ilikuwa imepangwa kuwa Baraza hilo litajwe leo lakini Ikulu jijini Paris imesema hatua hii imechukuliwa ili kumaliza uchunguzi wa Mawaziri wanaotarajiwa kuteuliwa.
Ripoti zinasema kuwa, kinachochunguzwa ni rekodi yao ya ulipaji kodi lakini pia kuthathmini ikiwa watakuwa na maslahi binafsi ikiwa watapewa nafasi hizo.
Pamoja na hilo, wachambuzi wa siasa nchini humo wanasema kuwa rais Macron anahitaji muda zaidi kuhakikisha kuwa Baraza lake linakuwa na uwakilishi wa pande zote za kisiasa.
Rais huyu mpya mwenye umri wa miaka 39, aliahidi kuunda serikali itakayowaleta pamoja wanasiasa wa Republican na Kisosholisti katika harakati za kuliunganisha kisiasa taifa hilo.
Macron ni rais aliyechaguliwa akiwa na msimamo wa kati, asiyeegemea siasa za mrengo wa kulia wala kushoto.
Siku ya Jumatatu, alimteua Edouard Philippe mwenye umri wa miaka 46 kuwa Waziri wake Mkuu.