UINGEREZA-USALAMA-MAUAJI

Polisi ya Uingereza yamtambua mtu aliyehusika na shambulio

Polisi ya Manchester yaendelea na uchunguzi katika eneo la tukio, Mei 23, 2017.
Polisi ya Manchester yaendelea na uchunguzi katika eneo la tukio, Mei 23, 2017. REUTERS/Darren Staples

Mshambuliaji aliyejitoa mhanga na kusababisha vifo vya watu 22 usiku wa Jumatatu katika mji wa Manchester, baada ya tamasha la muziki lililokua likitumbwizwa na mwanamuziki wa Marekani Ariana Grand anaitwa Salman Abedi, ambaye alikua na umri wa miaka 22, polisi ya Uingereza imetangaza Jumanne hii.

Matangazo ya kibiashara

"Naweza kuthibitisha kwamba mtu anayyeshukiwa kufanya ukatili wa usiku wa Jumatatu anaitwa Salman Abedi, mwenye umri wa miaka 22," Ian Hopkins, mkuu wa polisi katika mji wa Manchester, ameviambia vyombo vya habari. Aliongeza kuwa hataongeza lolote ziada kwa sasa kuhusu mtu huyo.

"Kipaumbele chetu, pamoja na polisi wa kupambana na ugaidi na washirika wetu katika idara za usalama, ni kuendelea kuchunguza na kujua kama alikua pekee yake au kama sehemu ya mtandao mpana," Ian Hopkins amesema.

Vyanzo vilivyo karibu na idara za usalama za Marekani, ambavyo vinanukuu wenzao wa Uingereza, vinaonyesha kuwa Salman Abedi alizaliwa katika mji wa Manchester mwaka 1994 kutoka kwa wazazi wenye asili ya Libya ambao walihamia London kabla ya kuhamia katika mji mkubwa wa kaskazini mwa Uingereza miaka kumi iliyopita.

Nyumba inayopatikana katika mji wa Fallowfield, ambapo familia ya kijana ilikua ikiishi wakati huo, katika kitongoji cha kusini mwa mji wa Manchester, ilifanyiwa msako Jumanne hii.

Mtu mwenye umri wa miaka 23 aliyekamatwa katika operesheni nyingine ya polisi siku ya Jumanne kama sehemu ya uchunguzi ni ndugu wa Salman Abedi, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Uingereza.