UINGEREZA-UGAIDI

Uingereza yasema haitatishwa na magaidi baada ya shambulizi la bomu mjini Manchester

Gari la kubeba wagonjwa katika mji wa Manchester baada ya shambulizi la bomu
Gari la kubeba wagonjwa katika mji wa Manchester baada ya shambulizi la bomu REUTERS/Andrew Yates

Viongozi mbalimbali duniani wamelaani shambulizi la kigaidi lililotokea mjini Manchester nchini Uingereza usiku wa kuamkia leo na kusababisha vifo vya watu 22 pamoja na watoto kadhaa na kuwaacha wengine 59 na majeraha.

Matangazo ya kibiashara

Waziri Mkuu Theresa May amelaani shambulizi hilo na kusema, haliwezi kuwagawa raia wa Uingereza kamwe.

Ameongeza kuwa imebainika kuwa aliyetekeleza shambulizi hilo alikuwa peke yake na aliuawa baada ya kujilipua kwa mujibu wa uchunguzi wa awali wa Polisi.

Imebainika kuwa bomu iliyotumiwa ilitengenezwa nyumbani huku kundi la Islamic State likidai kuhusika na shambulizi hilo.

Aidha May amesema kuwa magaidi hawawezi kushinda na wakati uo kutangaza kusitishwa kwa kampeni za kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi ujao.

“Hili ni shambulizi ambalo limetushtua sana lakini limeonesha uwoga wa magaidi ambao waliwalenga watu ambao hawakuwa wamejihami, watoto waliokuwa wanafurahia maisha yao,” amesema Waziri Mkuu May.

Naye rais wa Marekani Donald Trump akizungumza mjini Bethlehem katika ukingo wa Magharbi baada ya kukutana na rais wa Palestina Mahmud Abbas, amelaani shambulizi hilo na kuwataka magaidi kama watu wanaoshindwa.

“Nawaita watu walioshindwa, kwa sababu hivyo ndivyo walivyo. Tunao wengi, lakini wameshindwa, kumbukeni hilo,” alisema Trump.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amelaani shambulizi hili na kusema, nchi yake itaendelea kushirikiana na Uingereza kupambana na ugaidi, ahadi ambayo pia imetolewa na rais wa Urusi Vladimir Putin huku rais Emmanuel Macron akisema ameshtushwa na kushangazwa na shambulizi hili.

Shambulizi hilo lilitokea baada ya kumalizika kwa tamasha la muziki katika ukumbi wa Manchester Arena, baada ya mwimbaji kutoka Marekani Ariana Grande kuwaburudisha wafuasi wake.