UFARANSA-SIASA

Mshirika wa karibu wa rais wa Ufaransa akabiliwa na kashfa mpya

Waziri wa Mshikamano wa kitaifa, Richard Ferrand.
Waziri wa Mshikamano wa kitaifa, Richard Ferrand. RFI/ Pierre René-Worms

Richard Ferrand, mshirika wa karibu wa rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anakabiliwa na kashfa mpya ya udanganyifu.

Matangazo ya kibiashara

Siku ya Jumatano Mei 24, 2017, gazeti la kila wiki la Canard enchaîné limefichua kesi ya Pénélope Fillon, likibaini kwamba Waziri wa Mshikamano wa kitaifa, ambaye ni mshirika wa karibu wa Emmanuel Macron alitumia uongo kwa kukodi majengo ya mpenzi wake, alipokua Mkurugenzi Mkuu wa shirika moja nchini Ufaransa.

Kashfa hii mpya imezua hali ya sintofahamu katika serikali ya Ufaransa, ambayo inaandaa kuwasilisha sheria yake kuhusu maadili ya taifa.

Hata hivyo Richard Ferrand amejaribu kujitetea kuwa hajafanya kosa. Lakini kesi hii “imezua hali ya sintofahamu katika mazingira ya kutatanisha”, amekiri msemaji wa serikali, Christophe Castaner.

Tukio hili lilitokea mwaka 2011, wakati ambapo Richard Ferrand alikua bado hajajiunga katika siasa. Shirika la Mutuelles de Bretagne, alililokua akiongoza wakati huo, lilihamia kwenye majengo mapya, yaliyokodiwa kutoka kwa shirika lililokua limeanzishwa na mpenzi wake Sandrine Doucen.

Kwa mujibu wa gazeti la kila wiki la Canard enchaîné, Sandrine Doucen, alipokea mkopo wa benki wa 100% ya mauzo ya majengo hayo, kwa sababu alikua na ahadi ya kukodiwa majengo yake na shirika la Mutuelles de Bretagne, ambalo lililipa Euro 184,000 za shughuli za ukarabati wa eneo hilo.

Gazeti la kila wiki la Canard enchaîné limeongeza kuwa tangu mwaka 2011 kampuni ya Sandrine Doucen ilijikuta thamani yake “ikiongezeka mara 3000”.

Kashfa hii mpya inaibuka wiki moja tu baada ya serikali kuundwa. Hata hivyo serikali ya Emmanuel Macron imepuuzia mbali tuhuma hizo. Makada wa vuguvugu la En Marche! wamesema kuwa kesi hiyo haihusu serikali na ni mambo ambayo yalifanywa ya kampuni mbili binafsi, jambo ambalo haliingiliani na maadili ya taifa.