UINGEREZA-UGAIDI

Polisi nchini Uingereza wasitisha kubadilishana taarifa za Kiinteljensia kwa Marekani

Raia wa Uingereza wakiweka maua kuwakumbuka watu 22 waliopoteza maisha mjini Manchester
Raia wa Uingereza wakiweka maua kuwakumbuka watu 22 waliopoteza maisha mjini Manchester REUTERS/Peter Nicholls

Polisi nchini Uingereza wanasema wameacha kubadilishana taarifa za siri kwa Marekani kuhusu uchunguzi wa shambulizi la kigaidi lililotokea mjini Manchester siku ya Jumatatu usiku na kusababisha vifo ya watu 22 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 50.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hii imekuja baada ya Gazeti la Marekani la New York Times kuchapisha picha za shambulizi hilo na taarifa za siri zilizokuwa zimetolewa kwa maafisa wa Marekani.

Ripoti zinasema kuwa, Gazeti hilo lilichapisha taarifa za aliyetekeleza shambulizi hilo ambaye alibainika kwa jina la Salman Abedi. Polisi wanashuku kuwa hakuwa peke yake alipotekeleza shambulizi hilo.

Polisi wanasema hadi sasa wamewakamata washukiwa wanane wanaotuhumiwa kushirikiana na Salman aliyeuawa.

Waziri Mkuu Theresa May amesema atazungumza na rais Donald Trump wanapokutana katika mkutano wa NATO jijini Brussels nchini Ubelgiji, ili kumsisitizia umuhimu wa taarifa za  Kiintelejensia kuwa siri.

Uamuzi huu wa serikali ya Uingereza, sio wa kawaida kwa sababu mataifa haya mawili ambayo ni washirika wa karibu sana, mara kwa mara wamekuwa wakibadilishana taarifa za kiusalama.

Wakati uo huo, raia wa Uingereza wameendelea kutoa risala za rambirambi kwa jamaa ndugu na marafiki waliopoteza wapendwa wao huku Malkia Elizabeth wa Pili akiwatembelea waliojeruhiwa katika shambulizi hilo.