UINGEREZA-UGAIDI

Polisi nchini Uingereza wasema wanafahamu waliotekeleza shambulizi la kigaidi

Polisi wakilinda usalama katika daraja lililoshambuliwa jijini London Juni 2 2017
Polisi wakilinda usalama katika daraja lililoshambuliwa jijini London Juni 2 2017 REUTERS/Peter Nicholls

Polisi nchini Uingereza wanasema wanawafahamu magaidi watatu waliotekeleza shambulizi la kigaidi Jumamosi iliyopita jijini London nchini Uingereza na kusababisha vifo vya watu 7 na kuwajeruhi wengine 48.

Matangazo ya kibiashara

Wakuu wa usalama jijini London wamesema, watatoa majina yao hivi karibuni.

Waziri Mkuu Bi.Theresa May amesema nchi hiyo bado inakabiliwa na tishio la ugaidi, na hivyo maafisa wa usalama wanafanya kila kilicho ndani ya uwezo wao kuhakikisha kuwa shambulizi lingine halitokei tena nchini humo.

Kundi la kigaidi la Islamic State limejigamba kutekeleza shambulizi la pili la kigaidi kwa kipindi cha miezi miwili.

Wanasiasa wanarejelea kampeni zao kuelekea Uchaguzi Mkuu siku ya Alhamisi wiki hii, ushindani mkali ukitarajiwa kuwa kati ya chama cha Labour na Conservative.

Polisi wanasema wanawashikilia watu 11 kwa mahoajino zaidi kuhusu shambulizi hilo, huku rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akisema Paris, itaendelea kusimama na Uingereza katika vita dhidi ya ugaidi.

Watu hao walipoteza maisha baada ya kugongwa na gari katika daraja maarufu jijini London na kuwadunga visu watu wengine, huku washambuliaji hao wakipigwa risasi na kuuawa na polisi.