UINGEREZA

Watu sita wapoteza maisha kutokana na mkasa wa moto jijini London

Moto ulioteketeza jengo Magharibi mwa jiji la London
Moto ulioteketeza jengo Magharibi mwa jiji la London REUTERS/Toby Melville

Watu sita wamethibitishwa kupoteza maisha baada ya moto mkubwa kuteketeza jengo la orofa 24 Magharibi mwa jijini la London nchini Uingereza siku ya Jumanne usiku.

Matangazo ya kibiashara

Idadi kubwa ya watu wengi wamejeruhiwa na wanaendelea kupewa matibabu katika hospitali mbalimbali jijini humo.

Polisi na maafisa wengine wa uokoaji wanahofia kuwa huenda idadi na vifo ikaongezeka kwa sababu inaaminiwa kuwa kuna idadi kubwa ya watu ambao bado hawajapatikana.

Inahofiwa kuwa kuna idadi ya watu isiyofahamika waliokwama ndani ya jengo hilo ambalo kwa sasa limefunikwa na moshi mzito.

Meya wa jiji hilo Sadiq Khan amesema maafisa wa ukoaji wamefanikiwa, kuwaokoa idadi kubwa ya watu katika jengo hilo linalofahamika kama Grenfell Tower.

Kuna wasiwasi kuwa huenda likaporomoka kutokana na uharibifu mkubwa uliosababishwa na moto mkubwa.

Walioshuhudia mkasa huo wanasema, kulikuwa na moto mkubwa ambao hawajawahi kuona katika maisha yao.

Bado chanzo cha moto huo hakijabainika.

Waziri Mkuu Theresa May ameshindwa kuunda serikali mpya hivi leo baada ya mkasa huu wa moto ambao umeleta huzuni kubwa nchini Uingereza.