UFARANSA-SIASA

Chama cha rais Macron Republique en Marche, chashinda Uchaguzi wa wabunge

Namna rais Emmanuel Macron alivyopiga kura.
Namna rais Emmanuel Macron alivyopiga kura. Reuters

Chama cha rais wa Ufaransa Emmanuel Macron cha Republique en Marche,  kimepata ushindi mkubwa katika mzunguko wa pili wa Uchaguzi wa wabunge uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.

Matangazo ya kibiashara

Kati ya viti 557 vilivyowania, chama cha rais Macron kimepata ushindi wa zaidi ya viti 300.

Ushindi huu unamaanisja kuwa sasa rais Macron yupo katika nafasi nzuri ya kupitisha sera za serikali yake na kutekeleza ahadi alizozitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi.

Hata hivyo, ni uchaguzi  ulioshuhudia kuanguka kwa viongozi wengi wa kisiasa waliopoteza viti vyao. 

Mafanikio ya rais Macron yamekuja wakati idadi ya wapiga kura ikipungua hadi kufikia asilimia 44, baada ya wagombea wengi kujiondoa katika mzunguko wa pili wa Uchaguzi huo.

Chama kikuu cha upinzani National Front (FN) kimepata wabunge nane kati ya 577 katika bunge hilo jipya.

Kiongozi wake Marine Le Pen aliyewania urais na kushindwa, naye kwa mara ya kwanza amechaguliwa kuwa mbunge katika bunge la Ufaransa.

Awali alikuwa mbunge wa Bunge la Umoja wa Ulaya.

Licha ya ushindi wa chama cha rais Macron, kiongozi huyo wa upinzani amesema sio ushindi wa kishindo kwa sababu idadi kubwa ya wapiga kura hawakujitokeza kushiriki.

Baada ya Uchaguzi huo, sasa Waziri Mkuu Edouard Philippe anatakiwa kujiuzulu leo au kesho kabla ya kuunda serikali mpya ambayo  haitarajiwi kuwa na mabadiliko makubwa.

Mawaziri sita wa serikali waliofanikiwa kuchaguliwa katika uchaguzi huu ni pamoja na Christophe Castaner, Richard Ferrand, Bruno Le Maire, Annick Girardin, Mounir Mahjoubi na Marielle de Sarnez