UINGEREZA-UGAIDI

Uvamizi mwingine jijini London waleta madhara, mtu mmoja apoteza maisha

Polisi wakiwa wameweka uzio katika eneo ambalo basi liliwagonga watu Juni 19 2017 jijini London nchini Uingereza
Polisi wakiwa wameweka uzio katika eneo ambalo basi liliwagonga watu Juni 19 2017 jijini London nchini Uingereza s.yimg.com

Mtu mmoja amepoteza maisha na wengine wamejeruhiwa Kaskazini mwa jiji la London nchini Uingereza baada ya basi dogo kuwagonga waumini wa dini ya Kiislamu waliokuwa wanatoka msikitini usiku wa kuamkia siku ya Jumatatu.

Matangazo ya kibiashara

Baraza la Waislamu nchini humo limethibitisha kutokea kwa tukio hilo wakati huu Waislamu wakiwa kwenye mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Waziri Mkuu Theresa May amelaani kilichotokea na kusema inasikitisha.

Aidha ameeleza kuwa maafisa wa usalama wanachunguza kubaini ikiwa lilikuwa ni tukio la kigaidi.

Dereva wa basi hilo amekamatwa na anahojiwa zaidi.

Mwezi uliopita, watu kadhaa walipoteza maisha na wengine kujeruhiwa baada ya gari kuwagonga wapita njia katika daraja maarufu katika jiji hilo, shambulizi ambalo kundi la Islamic State lilidai kutekeleza.

Mkasa huu pia umekuja baada ya wakaazi wa jiji hilo kuomboleza vifo vya zaidi ya watu 50 walioteketea wakiwa ndani ya jengo la makaazi na kusababisha majeraha mengine.