ULAYA-MACRON-DEMOKRASIA

Emmanuel Macron atetea demokrasia halisi kwa Ulaya

Emmanuel Macron ahutubia kwenye mlima wa Pnyx nchini Ugiriki, Septemba 7, 2017.
Emmanuel Macron ahutubia kwenye mlima wa Pnyx nchini Ugiriki, Septemba 7, 2017. REUTERS/Aris Messinis/Pool

Uanzishwaji upya wa Ulaya ni moja ya miradi mikubwa ya rais wa Ufaransa Emmanuel Macron. Rais wa Ufaransa alitumia safari yake kwenda mjini Athens, nchini Ugiriki, nchi ambayo ni kitovu cha demokrasia, ili kutoa siku ya Alhamisi Septemba 7 maono yake kuhusu mustakabali wa Ulaya.

Matangazo ya kibiashara

Katika kuzindua mradi wake wa "kuanzisha upya kidemokrasia Ulaya" mjini Athens,rais Macron amejiuliza maswali mengi kuhusu hatama ya Ulaya iwapo hali itaendelea kama ilivyo.

Rais wa Ufaransa alianza hotuba yake kwa maneno machachekwa lugha ya Kigiriki ili kusisitiza "fursa kubwa" ya kuwa nchini humo. "Tumefanya nini kwa demokrasia yetu, tumefanya nini na uhuru wetu? Leo, uhuru, demokrasia na imani viko hatarini, " alisema Emmanuel Macron. Kwa mtazamo wake, demokrasia imekosekana Ulaya kwa zaidi ya miaka kumi iliyopita na anataka ifufuliwe upya.

Rais Macron amesema viongozi wa Ulaya wanapaswa kuwasilisha mapendekezo yao ifikapo mwishoni mwa mwaka, yatayofungua mjadala kwa wananchi kuamua ni aina gani ya muungano wanaouhitaji.

Macron ameahidi kuwasilisha mapendelezo yake ndani ya wiki chache zijazo, huku akisema itahusisha njia za kidemokrasia zaidi ikiwemo bunge la nchi yake.

Rais wa Ufaransa anataka "kwa pamoja" kupata "nguvu za kujenga upya Ulaya". Ulaya yenye nguvu, Ulaya huru, yenye uwezo wa kukabiliana na migogoro bila kuingiliwa nchi za kigeni, Ulaya ambayo itakua na nguvu zake za awali, ni Ulaya hiyo ambayo kiongozi wa Ufaransa anataka.