CATALONIA-UHISPANIA-HAKI

Uhispania yamuitisha Puigdemont kujibu mashitaka yanayomkabili

Aliyekua rais wa Catalonia, Carles Puigdemont.
Aliyekua rais wa Catalonia, Carles Puigdemont. REUTERS/Ivan Alvarado

Serikali kuu ya Uhispania imemtaka aliyekua rais wa Catalonia, Carles Puigdemont, kurejea nyumbani kujibu mashitaka yanayomkabili.

Matangazo ya kibiashara

Bw. Puigdemont anashtumiwa kuanzisha uasi dhidi ya serikali kuu ya Uhispania.

Tuhuma hizi zimekuja siku chache baada ya Carles Puigdemont kufutilia mbali uamuzi uliochukuliwa na serikali kuu ya Uhispania ya kumtimua kwenye wadhifa wake na kuziweka taasisi zote za eneo hilo lililokua likijitawala chini ya mamlaka yake.

Carles Puigdemont, ambaye yuko Ubelgiji amesema atarudi nchini Uhispania kama serikali ya nchi hiyo itaacha vitisho vya kumshikilia kwa muda mrefu.

Awali Bw. Puigdemont alisema kuwa ataendelea na msimamo wake licha ya vitisho vya serikali kuu ya uhispania.

Wakati huo huo Mahakama Kuu nchini Uhispania imetaka kufikishwa Mahakamani kwa aliyekuwa kiongozi wa jimbo la Catalonia Carles Puidgemont na watu wengine 13, wiki hii.

Aidha, Mahakama imewapa siku tatu kulipa dhamana ya Dola Milioni 7.2.

Mapema wiki hii, Ubelgiji ilisema iko tayari kumpa hifadhi ya ukimbizi aliyekuwa rais wa Catalonia, Carles Puigdemont.