UINGEREZA-ISRAEL-USHIRIKIANO-SIASA

Waziri mwengine ajiuzulu Uingereza

Waziri mwengine amejiuzulu kwenye serikali ya May, Uingereza.
Waziri mwengine amejiuzulu kwenye serikali ya May, Uingereza. REUTERS/Maurizio Degl'Innocenti

Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza, Priti Patel, alitangaza kujiuzulu siku ya Jumatano usiku baada ya kukutana na viongozi wa kisiasa wa Israeli bila kujulisha serikali yake.

Matangazo ya kibiashara

Priti Patel amekua afisa wa pili kuondoka kwa baraza la mawaziri ndani ya kipindi cha wiki moja, vyanzo vya serikali vimesema.

Priti Patel, mwenye umri wa miaka 45, aliomuomba msamaha Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May na kuomba kujiuzulu baada ya kuitishwa siku ya Jumatano katika Ofisi ya Waziri Mkuu, na hivyo, kusitisha ziara yake barani Afrika.

"Nilifanya hivyo kwa nia njema, lakini matendo yangu hayakuheshimu mahitaji ya uwazi ambayo nililitetea," Priti Patel aliandika kwenye barua yake ya kujiuzulu.

"Uingereza na Israeli ni washirika wa karibu na ni sawa tufanye kazi kwa pamoja. Lakini hili linapaswa kufanyika kwa njia rasmi, kupitia njia zinazojulikana kiserikali," Theresa May aliandika akimjibu.

Priti Patel amekua waziri wa pili kuacha kazi ndani ya kipindi cha wiki moja baada ya Waziri wa Ulinzi Michael Fallon Novemba 1. Bw. Fallon alihusishwa katika kashfa ya unyanyasaji wa kijinsia inaendelea kuwakabili viongozi wa kisiasa nchini Uingereza na kutishia pia kumfanya ajiuzulu mshirika wa karibu wa Theresa May, Naibu Waziri Mkuu Damian Green, na Waziri wa Biashara ya Kimataifa Mark Garnier.

Bi Patel alikuwa ameomba msamaha siku ya Jumatatu kwa kukutana na maafisa kadhaa wa Israeli, ikiwa ni pamoja na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, na wawakilishi wa shirika moja lisilo la kiserikali namakampuni mbalimbali wakati wa likizo yake mwezi Agosti bila kujulisha mapema serikali yake.