UGIRIKI-MAJANGA YA ASILI-USALAMA

Watu zaidi ya 40 wafariki dunia kwa mkasa wa moto Ugiriki

Moto uliozuka karibu na Rafina, kilomita 55 kutoka Athens, usiku wa Tarehe 23 kuamkia 24 Julai 2018.
Moto uliozuka karibu na Rafina, kilomita 55 kutoka Athens, usiku wa Tarehe 23 kuamkia 24 Julai 2018. REUTERS/Alkis Konstantinidis

Watu zaidi ya 40 wamefariki dunia kwa mkasa wa moto mkubwa uliozuka na kuunguza msitu nchini Ugiriki. Serikali nchini Ugeriki imetolea wito jumuiya ya kimataifa kusaidia kukabiliana na moto huo ambao umeunguza msitu na kufanya uharibifu mkubwa nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Kikosi cha uokoaji kinaendelea na jitihada za kuwapata watalii 10 ambao walitoweka katika harakati za kujiokoa na moto huo.

Mamia ya wafanyakazi wa vikosi vya zima moto,wanaendelea na jitihada za kuuzima moto huo.

Kwa mujibu wa vyanzo vya polisi watu kadhaa wameyatoroka makazi yao katika maeneo yalio karibu na mji mkuu wa taifa hilo Athens.

Waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras, ambaye amelazimika kukatisha ziara yake ya Bosnia ili kusaidia uratibu wa hali hiyo, amesema watafanya kilio chini ya uwezo wao kuhakikisha wanaokoa maisha ya watu.

Waziri mkuu Tsipras amesema hali ya hatari imetangazwa katika Attica karibu na mji wa Athens.

Awali msemaji wa serikali Dimitris Tzanakopoulos alisema kuwa watu 20 walifariki dunia kwa mkasa huo wa moto.

Nchi za Italia, Ujerumani, Poland na Ufaransa wametuma misaada ya ndege, magari na watalaamu wazima moto kusaidia kukabiliana na moto huo.

Kwa mujibu wa mashahidi watu 104 wamejeruhiwa kati yao 11 wakiwa katika hali mbaya, lakini watoto 16 nao wamejeruhiwa.